Mtafiti Mkuu katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi za Afya Muhimbili (MUHAS) Prof. George Ruhago akizungumza katika warsha ya wadau wa sekta ya afya iliyofanyika leo Oktoba mosi 2025 katika hotel ya White Sand Jijini Dar es Salaam.
Mtaalamu wa uchumi wa afya, Dkt. Friday Ngaleson, akizungumza na washiriki wa katika warsha ya wadau wa sekta ya afya.
Prof Mfinanga Sayoki akizungumza na washiriki wa katika warsha ya wadau katika sekta ya afya.
Wadau wa sekta ya afya wakiwa katika warsha
……………..
Mtafiti Mkuu kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Prof. George Ruhago, amesema kuwa mapendekezo ya utekelezaji wa mfumo wa huduma jumuishi wa “moja kwa moja” kwa kuunganisha huduma za VVU/UKIMWI na magonjwa yasiyo ya kuambukiza (NCDs) yanatarajiwa kuboresha utoaji wa huduma na matumizi ya rasilimali kwa ufanisi zaidi.
Akizungumza katika mkutano wa kiwango cha juu wa wadau wa sekta ya afya uliofanyika Oktoba 1, 2025, jijini Dar es Salaam Prof. Luhago ameeleza kuwa mfumo huu mpya utawawezesha wagonjwa kupata huduma zote muhimu kwa pamoja.
Prof. Ruhago amesema kuwa mkutano huo umewaleta pamoja wataalamu mbalimbali kwa lengo la kuboresha ramani ya utekelezaji, kushiriki matokeo ya tafiti, pamoja na kuweka mikakati ya uhamasishaji wa rasilimali na utoaji wa huduma kwa njia endelevu.
Prof. Ruhago amefafanua kuwa chini ya mfumo huu, wagonjwa wataweza kutibiwa VVU, kisukari, shinikizo la damu na magonjwa mengine kwenye kituo kimoja, chini ya usimamizi wa timu moja ya huduma.
“Wagonjwa hawatahitaji tena kuhudhuria kliniki tofauti kwa kila hali. Huduma zitapatikana mahali pamoja na kupitia mfumo mmoja wa uchunguzi na tiba,” amesema.
Mpango huu wa huduma jumuishi unaungwa mkono na taasisi mbalimbali za kimataifa zikiwemo Chuo Kikuu cha Harvard, Chuo Kikuu cha Boston na mashirika ya maendeleo.
Prof. Ruhago ameongeza kuwa kipengele muhimu cha mfumo huu ni matumizi ya mbinu ya Usimamizi na Upimaji wa Gharama Kulingana na Shughuli (ABC/M), inayolenga kufahamu gharama halisi ya kila huduma ili kuwezesha uamuzi bora wa sera.
“Kwa kutumia ABC/M, tunaweza kufuatilia gharama na matokeo kwa wakati halisi, jambo linalosaidia kutenga rasilimali kwa ufanisi zaidi na kuondoa matumizi yasiyo ya lazima,” amesema.
Hatua za awali za utekelezaji wa mfumo huu ni pamoja na kuanzisha kliniki za huduma jumuishi katika maeneo mbalimbali nchini, sambamba na kupitia upya sera za malipo na fidia ili zilingane na mfumo mpya.
Kwa upande wake, Mtaalamu wa Uchumi wa Afya, Dkt. Friday Ngaleson, ameeleza kuwa tafiti zinaonyesha kuwa kuunganisha huduma hakusababishi ongezeko kubwa la gharama, bali huboresha ufanisi na matokeo ya afya kwa kiasi kikubwa.
“Huu si mabadiliko ya kiufundi tu, bali ni mageuzi makubwa katika namna tunavyotoa huduma za afya,” amesema.
Naye , Rais wa Chama cha Madaktari wa Kisukari Tanzania (TDA), Prof. Ramaiya Kaushik, amesema kuwa mfumo huu utamuwezesha mgonjwa kuhudumiwa na mtaalamu mmoja aliyehitimu, jambo litakalorahisisha ufuatiliaji na utunzaji bora wa afya.