Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema endapo atapewa ridhaa ya kuunda serikali kupitia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, serikali yake itajenga tawi la Chuo cha Biashara (CBE) katika Wilaya ya Hai, Mkoa wa Kilimanjaro, ili kuongeza fursa za elimu mkoani humo na kuimarisha uchumi wa Wilaya ya Hai.
Dkt. Samia ameyasema hayo leo Jumatano, Oktoba 1, 2025, wakati akizungumza na maelfu ya wananchi waliofurika katika Viwanja vya Mashujaa, Moshi Mjini, katika siku yake ya pili ya kampeni mkoani humo. Alisisitiza kuwa ataendeleza sera ya elimu bila malipo pamoja na kujenga vyuo vya VETA katika kila wilaya na mkoa nchini.
Vilevile, Dkt. Samia amezungumzia maendeleo yaliyopatikana kwenye sekta ya maji nchini, akibainisha kuwa serikali inaendelea na awamu ya pili ya Mradi wa Maji wa Same–Mwanga–Korogwe ili kuhakikisha maji yanawafikia vijiji vya pembezoni mwa wilaya hizo. Aidha, alieleza kuhusu ujenzi wa mradi wa maji kutoka Ziwa Chala kwenda Wilaya ya Rombo kwa gharama ya Shilingi Bilioni 9.8, pamoja na mradi wa maji Wilaya ya Siha utakaogharimu takribani Shilingi Bilioni 14 na kuhudumia vijiji nane vya wilaya hiyo.