*Asema Serikali kuwa lishe ni nguzo ya maendeleo ya rasilimali watu, uchumi na jamii
*Asema kiwango cha uzito uliozidi na uzito kupita kiasi hasa wanawake wa umri wa kuzaa kimeongezeka
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema kuwa kiwango cha udumavu miongoni mwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano nchini kimeshuka kutoka asilimia 48 mwaka 1992 hadi asilimia 30 mwaka 2022.
Ameongeza kuwa, kiwango cha ukondefu miongoni mwa watoto walio chini ya miaka mitano kimepungua kutoka asilimia 5 mwaka 1992 hadi asilimia 3.2 mwaka 2022.
Amesema hayo leo Jumanne (Septemba 30, 2025) wakati alipofunga mkutano wa 11 wa wadau wa lishe nchini, uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa APC uliopo Bunju Jijini Dar es salaam.
Amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inatambua kuwa lishe si suala la kiafya pekee, bali ni nguzo ya maendeleo ya rasilimali watu, uchumi na jamii. “Dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa na chakula cha kutosha, afya njema na lishe bora”
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Rais Dkt. Samia ameendelea kuwa kinara wa mapambano dhidi ya utapiamlo kwa kuhakikisha masuala ya lishe yanapewa kipaumbele kwa kuimarisha bajeti, kuboresha mifumo ya ufuatiliaji na uhamasishaji wa afua za lishe kuanzia ngazi ya taifa hadi vijijini.
“Jitihada hizi zilimuwezesha kupata tuzo ya Global Goalkeeper kutoka Taasisi ya Gates Foundation, kutokana na mchango wake mkubwa katika kusukuma mbele Malengo ya Maendeleo Endelevu, hususan kwenye afya ya mama, mtoto na lishe”.
Katika hatua nyingine, mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa kiwango cha uzito uliozidi na uzito kupita kiasi (kiribatumbo) hasa miongoni mwa wanawake wa umri wa kuzaa kimeongezeka kutoka asilimia 28 mwaka 2015 hadi asilimia 37 mwaka 2022. “Changamoto hii inaakisi mabadiliko ya ulaji na mtindo wa maisha ulioikumba sio tu Tanzania bali dunia nzima“.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa Wizara na Taasisi zote za umma na binafsi kutenge rasilimali za kutosha kwa ajili ya afua za lishe na kuziweka katika mipango yao ya kila mwaka ili kuongeza uwajibikaji na uendelevu katika kutekeleza mipango iliyopangwa.
Pia Mheshimiwa Majaliwa amezitaka Taasisi za Utafiti na Vyuo vya Elimu ya juu kuendeleza tafiti katika masuala ya lishe pamoja na kuhakikisha ripoti za tafiti hizo zinatumika kuboresha sera na mikakati nchini.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana Ajira na Wenye Ulemavu)Ridhiwan Kikwete amesema kuwa Serikali itahakikisha kuwa wadau wote walioanishwa katika Mpango Jumuishi wa masuala ya Lishe wanaendela kutekeleza majukumu yao. “Hii ni pamoja na kuhakikisha kuwa Wizara zote zinaingiza masuala ya lishe katika mipango ya kibajeti kila mwaka”
Ameongeza kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu imefanikiwa kukamilisha zoezi la utafiti wa gharama za utapiamlo ambao ulilenga kubainisha gharama na athari za utapiamlo katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi
“Matokeo ya utafiti huo yatatumika kama nyenzo muhimu ya uhamasishaji wa viongozi wa juu wa Serikali na watunga sera, kupitia majukwaa mbalimbali ili kuchangia hatua zaidi katika mapambano ya kutokomeza utapiamlo hasa kwa watoto”