NA JOHN BUKUKU – KOROGWE
Mgombea Urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kwamba katika kipindi cha miaka mitano ijayo watahakikisha viwanda vilivyobinafsishwa na havifanyi kazi vinapatiwa wawekezaji wengine na kukabidhiwa kwa Ushirika chini ya usimamizi wa Serikali.
Dkt. Samia aliyasema hayo leo wakati akizungumza na wananchi wa mji wa Korogwe katika mkutano wake wa kampeni ambapo alisema kwa wilaya ya Korogwe kuna mashamba ambayo hayaendelezwi na watu wanayaangalia.
Alisema kwamba tayari ameelekeza Wizara ya Kilimo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wayafanyie kazi, waangalie mikataba yao na wawekezaji ili kuona namna ya kuivunja mikataba hiyo, mashamba yarudi serikalini na Serikali iweze kufanya maamuzi mengine.
Aidha, alisema pia kwa upande wa kiwanda cha chai watakwenda kuweka mitambo mipya. Alifafanua kuwa licha ya kiwanda kilichofungwa, Serikali itaweka mitambo mingine ya kuchakata zao la chai, na kiwanda hicho kitaendeshwa chini ya Ushirika wa Chai Korogwe na kusimamiwa na Bodi ya Chai.
Akizungumzia mashamba ya mkonge ya Sisalana, Dkt. Samia alisema mashamba hayo ambayo wenyewe hawaonekani hayajaendelezwa ipasavyo na uchakataji wa mkonge umedorora. Alieleza kuwa Serikali imeitaka NSSF kupitia Wizara ya Kilimo kufanya tathmini ya mashamba na kiwanda, lengo likiwa ni kuongeza uwezo wa kuchakata kwa kufunga mitambo mipya.
Alisema kwamba mitambo hiyo itaendeshwa chini ya Amcos ya Mkonge na kusimamiwa na Bodi ya Mkonge, huku akigusia pia Kiwanda cha Kamba cha Tancod ambacho kitafanyiwa tathmini kwa kuangalia uwezekano wa kumpata mwekezaji mwingine mwenye uwezo wa kukiendesha vizuri.
Hata hivyo, alisema kwamba endapo hakutapatikana mwekezaji mwingine, Serikali itakichukua kiwanda hicho na kukiendesha chini ya ushirika. Alisisitiza kuwa Serikali imeimarisha sekta ya ushirika nchini na sasa inaweza kusimamia shughuli zake kwa ufanisi.