βNA JOHN BUKUKU- KOROGWE
Mkazi wa Korogwe Vijijini, Bi. Khadija Mshahara, amezungumzia kazi kubwa ya maendeleo iliyotekelezwa na Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika jimbo hilo.
Bi. Khadija amesema kuwa Dkt. Samia amefanya mambo makubwa katika kipindi chake, akibainisha kuwa miradi yote ya kimkakati iliyoachwa na mtangulizi wake imetekelezwa, ikiwemo Bwawa la Mwalimu Nyerere na mingineyo.
Akizungumzia sekta ya afya, amesema wilaya ya Korogwe kwa sasa ina zahanati mpya 6 zinazohudumia wananchi, huku akiongeza kuwa zipo zahanati nyingine 6 zinazotarajiwa kujengwa katika kipindi cha miaka 5 ijayo.
Katika sekta ya elimu, Bi. Khadija amesema shule 11 za sekondari zimejengwa katika wilaya ya Korogwe. Aidha, akibainisha kuwa katika sekta ya maji, Dkt. Samia ametekeleza miradi ya kimkakati zaidi ya mitano ikiwemo mradi wa Mombo kupitia Mto Ruvu.
Pia, katika mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na serikali, ameeleza kuwa kijiji cha Mombo pekee vikundi zaidi ya 6 vimenufaika, huku Korogwe Vijijini vikundi zaidi ya 45 vikipewa mikopo hiyo.
Bi. Khadija ametoa wito kwa wasimamizi wa uchaguzi na serikali kuhakikisha kunakuwepo na usafiri kwa wazee na watu wenye ulemavu ili waweze kufika katika vituo vya kupiga kura na kumchagua Dkt. Samia.
Aidha, amebainisha kuwa Dkt. Samia ni chaguo la wananchi wa Tanga, akisema hawana chaguo jingine.
Kwa upande wake, mmoja wa wakazi wa Mombo amesema wamepokea kwa faraja uamuzi wa serikali kuwaruhusu wananchi kuchukua miili ya wapendwa wao kwa ajili ya mazishi na kurejea kulipa gharama baadae.
Aidha, amesema kuwa atawahamasisha wanafamilia wote kwenda kumpigia kura Dkt. Samia pamoja na wagombea wa ubunge na udiwani.