Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
Mkoa wa Pwani umeendelea kuwa mfano wa mafanikio katika utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF), ikiwa ni sehemu ya jitihada za serikali kupunguza umasikini uliokithiri na kuboresha maisha ya wananchi wa kipato cha chini.
Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia uchumi na uzalishaji kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Shangwe Twamala, aliwaasa waratibu wa mpango huo kuhakikisha kuwa vikundi vilivyoundwa na kunufaika na TASAF awamu ya pili vinasimamiwa ipasavyo.
Aidha alihimiza wapewe elimu, mitaji na fursa kupitia mikopo ya asilimia 10 kutoka mapato ya Halmashauri, ili kuwawezesha kusimama kiuchumi na kuepuka kurejea katika hali ya umasikini.
Twamala alitoa wito huo leo, Septemba 30,2025 wakati akifungua kikao kazi cha mwaka cha Utekelezaji wa Mpango wa TASAF III Awamu ya Pili, kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Kibaha.
Aliishukuru Serikali kwa kutoa zaidi ya sh bilioni 44 kwa ajili ya kuendesha na kuwezesha miradi mbalimbali chini ya mpango huo.
Alisema mpango huo umeleta manufaa makubwa kwa familia zenye hali ngumu za kiuchumi, hasa kwa kuboresha huduma za jamii na kuinua vipato vya kaya.
Kwa mujibu wa Shangwe ni muhimu miradi yote inayotekelezwa kukamilika kwa wakati ili iweze kuwanufaisha walengwa na kuendana na dhamira ya serikali ya kuwainua wananchi.
Kwa upande wake, Mhandisi Abel Bimbiga, Mwakilishi kutoka Makao Makuu ya TASAF, aliupongeza mkoa wa Pwani kwa kuwa miongoni mwa mikoa inayotekeleza mpango huo kwa mafanikio makubwa.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mpango huo, Mratibu wa TASAF Mkoa wa Pwani, Roseline Kimaro, alieleza Mkoa wa Pwani ulikuwa miongoni mwa maeneo ya kwanza kufanya majaribio ya awali ya mpango huo, ambapo Wilaya za Bagamoyo na Kibaha ziliteuliwa kuanza utekelezaji wa awamu ya kwanza.
Kimaro alisema ,mkoa umetekeleza miradi mbalimbali ya afya na elimu katika maeneo 16, ikiwemo jengo la mochwari katika Hospitali ya Wilaya ya Msoga, wodi ya mama na mtoto katika Kituo cha Afya Miono, Chalinze, Zahanati ya Mwanalugali, Nyumba za watumishi katika Zahanati ya Vikawe wilayani Kibaha, Majengo matano katika Kituo cha Afya Nyamatanga wilaya ya Kibiti na Bweni la wasichana na nyumba za walimu katika Shule ya Sekondari Samia wilayani Rufiji.
Kufuatia mafanikio ya awali, serikali ilipanua TASAF hadi kufikia wilaya zote nchini na mikoa yote 26 ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wananufaika na juhudi za kupunguza umasikini.
Kimaro anasema hadi kufikia Juni 2025, Mkoa wa Pwani ulikuwa umeunda jumla ya vikundi 1,601 vya wanufaika, vyenye wanachama 16,495, kati yao, 14,568 ni wanawake na 1,927 ni wanaume, kupitia vikundi hivyo, wanufaika wameanzisha miradi ya kiuchumi, kuweka akiba na kujiimarisha kiuchumi.
“Wanufaika wamepata mafanikio makubwa katika huduma za msingi kama vile elimu, afya, lishe, makazi bora, na shughuli za kilimo, ufugaji, biashara ndogondogo, usindikaji wa bidhaa, ushonaji na ufumaji.
Kimaro alibainisha kuwa jumla ya mtaji wa vikundi hivyo umefikia sh milioni 330 hadi sasa.
“Lengo la serikali kupitia TASAF, si kutoa msaada wa muda mfupi pekee, bali ni kuwawezesha walengwa kuwa na msingi madhubuti wa kiuchumi na kuweza kujitegemea hata baada ya mpango kumalizika.
Anaeleza mafanikio haya ni matokeo ya ushirikiano wa karibu kati ya Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, viongozi wa jamii na wanufaika wenyewe, na kueleza matumaini kuwa mpango huo utaendelea kubadilisha maisha ya wananchi na kuchochea maendeleo endelevu ya Mkoa wa Pwani na taifa kwa ujumla.