Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Mgombea Ubunge wa Jimbo la Mtama Nape Nauye amesema kuwa tathmini ya uongozi inaonesha wazi kuwa Rais Samia Suluhu Hassan aendelee kuongoza nchi kwa sababu ameweza, na siyo kwa sababu ya utamaduni wetu. Amesema hatua hiyo ndiyo msingi wa chama kuamua kuendelea naye, kwani amekuta nchi ikikusanya shilingi trilioni 18 kwa mwaka na kwa usimamizi wake mzuri na uzalendo mkubwa, amesimamia ukusanyaji huo na kufanikisha kufikia shilingi trilioni 31 kutoka trilioni 18.
Ameyasema hayo leo wakati akizungumza kwenye mkutano wa kampeni wilayani Pangani mkoani Tanga, wa kumnadi mgombea urais kupitia CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Sasa hizo fedha ndiyo hizo ambazo mmeona zimekuja kwenye miradi mbalimbali ikiwemo maji, barabara, afya na ajira. Wote walioguswa na fedha hizi Oktoba 29 tuna kazi moja ya kutiki,” amesema.
Amesema kuwa, Mama Samia alipoingia madarakani, idadi ya ukaguzi ilikuwa haizidi 900, jambo lililosababisha changamoto kubwa za hati. Lakini kwa msimamo wake, akaagiza kuongezwa hadi kufikia ukaguzi 1,300. Hata hivyo, ukaguzi wa mwisho uliofanyika katika hati hizo 1,300 umeonesha asilimia 99 ya hati hizo ni safi na zinaridhisha.
Ameongeza kuwa, Rais Samia amesimamia mapato na kudhibiti matumizi, jambo lililopelekea hata ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kumpa pongezi.
Aidha, amefafanua kuwa Rais Samia ni muumini wa utu wa binadamu, jambo lililomsukuma kuunda Tume ya Rais ya kushughulikia haki jinai. Amesema Tanzania ina sheria mbalimbali za kusimamia haki za jinai tangu tupate uhuru, lakini kutokana na dhamira ya Mama Samia, tume hiyo iliundwa ili kuboresha na kusimamia zaidi haki hizo.
Nape ameongeza kuwa, Mama Samia alipoingia madarakani alikuta idadi ya vifo vya akinamama wakati wa kujifungua ikiwa zaidi ya 556 kati ya vizazi hai 100,000. Lakini kupitia hatua madhubuti, amefanikisha kushusha idadi hiyo kutoka 556 hadi kufikia 114. “Nani kama Mama Samia? Halafu leo mtu aseme Oktoba 29 tusitiki? Wananchi wanajua wanakwenda kutiki kwa utu wa mama huyu,” amesema.
Amesema pia, Mama Samia alipoingia madarakani alikuta akinamama wengi wakitegemea kuni na mkaa kwa kupikia, jambo lililokuwa hatarisha maisha yao. Ameanzisha kampeni ya nishati safi ya kupikia ambayo imeongeza matumizi kutoka asilimia 6 hadi asilimia 20. “Dunia imekubali na Afrika imekubali. Wewe usiyetaka kukubali umechanganyikiwa au unataka kujikoroga mwenyewe?” alihoji Nape.
“Nimesimama kuwaomba wananchi wa Pangani. Sisi tumejiridhisha, ndiyo maana tukamleta kwenu. Ninaamini Oktoba 29 tutawapuuza wote wanaotushawishi tusiende kupiga kura. Twendeni tukapigie kura maemdeleo,” amesema Nape.
Amefafanua zaidi kuwa, Mama Samia amefanikisha kazi zake bila mashaka. “Wanaobisha waje wapingane na takwimu hizi. Kama mtu yupo tayari kuokoa roho za akina mama na watoto waliokuwa wanapotea, kama siyo utu ni nini? Nawaombeni sana wananchi wa Pangani Oktoba 29 mkirudishe tena chama chetu madarakani,” amehitimisha.