NA JOHN BUKUKU, TANGA
Mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuufungua Mkoa wa Tanga kiuchumi kwa kuendelea kutekeleza miradi ya kimkakati itakayoongeza fursa za kiuchumi na kunufaisha wananchi wa mkoa huo.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika leo Septemba 29, 2025 kwenye Viwanja vya Usagara, jijini Tanga, Dkt. Samia alisema kuwa Bandari ya Tanga inatarajiwa kuwa kitovu cha usafirishaji wa mafuta na gesi, hatua itakayochochea uzalishaji wa ajira mpya zipatazo 2,001 na kukuza uchumi wa mkoa huo.
Aidha, alibainisha kuwa utekelezaji wa mradi wa kimkakati wa bomba la mafuta ghafi kutoka Uganda hadi Tanga umefikia asilimia 84, huku watu zaidi ya 2,000 wakiwa wameajiriwa katika Mkoa wa Tanga kupitia mradi huo.
Ameongeza kuwa Serikali imepanga kuanza ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Tanga kupitia Arusha hadi Musoma, mradi ambao unalenga kufungua fursa za uwekezaji katika sekta ya viwanda na madini.
Katika hatua nyingine, Dkt. Samia alisema barabara ya Handeni hadi Singida imeunganishwa na Bandari ya Tanga ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo, huku akisisitiza dhamira ya Serikali kuunganisha mkoa huo na Pwani kwa lengo la kuongeza fursa za kiuchumi.
“Tutafanya upanuzi na ukarabati wa barabara kuu ya Dar es Salaam, Chalinze, Arusha ili kupunguza msongamano na kuimarisha Tanzania ya viwanda, kwa kuwa huu ni mkakati wa Taifa,” alisema Dkt. Samia.
Ameeleza kuwa Serikali inalenga kufufua viwanda vyote vya Mkoa wa Tanga na kuwahamasisha wawekezaji kuwekeza katika mkoa huo, jambo litakalosaidia kuongeza ajira kwa vijana.
Katika sekta ya madini, alisema masoko ya dhahabu yameanzishwa ili kuwavutia wawekezaji na kuwawezesha wachimbaji wadogo kunufaika na ongezeko la upatikanaji wa masoko.
Kuhusu kilimo, Dkt. Samia alisema Serikali imejipanga kuboresha sekta hiyo kwa kuimarisha kilimo cha umwagiliaji ili kuongeza tija, pamoja na kujenga soko la kisasa kwa wamachinga litakalogharimu shilingi bilioni 1.9 na kuwa na uwezo wa kuchukua wafanyabiashara 1,400.
“Tunakwenda kujenga soko la kimataifa la samaki ili wavuvi wetu waweze kufanya kazi katika mazingira rafiki,” ameongeza.
Akizungumzia sekta ya afya, alisema Serikali imejenga zahanati na vituo vya afya katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Tanga. Pia ametangaza kuwa huduma ya afya bure itaanza kutolewa kwa wananchi wote wa mkoa huo kama sehemu ya majaribio.
“Tutaanzia Tanga kwa majaribio, ambapo wananchi watapata matibabu bure na kuondokana na changamoto ya miili ya marehemu kuzuiliwa kutokana na deni la matibabu,” alisema.
Kwa upande wa elimu, Dkt. Samia alisema Serikali itaendelea na sera ya elimu bila malipo, sambamba na kuwekeza katika miundombinu ya elimu kuanzia ngazi ya shule za msingi, sekondari hadi vyuo, ili kila Mtanzania apate elimu kulingana na uwezo wake.
Pia alisema Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya maji katika Mkoa wa Tanga kwa lengo la kuhakikisha kila Mtanzania anapata maji safi na salama.
Katika sekta ya nishati, Dkt. Samia alisema Serikali inalenga kuhakikisha kila Mtanzania anatumia nishati safi inayotokana na maji, upepo, gesi na jua, na kuwa miradi ya kuzalisha na kusambaza umeme inaendelea kutekelezwa ili kuwasaidia wananchi wa vijijini kunufaika na huduma hiyo, ambapo Serikali imetoa bei maalum za umeme.