NA JOHN BUKUKU-CHALINZE
Mgombea ubunge wa Jimbo la Chalinze, Ridhiwan Kikwete, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa ya maendeleo iliyotekelezwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita katika Halmashauri ya Chalinze.
Ameyasema hayo Septemba 28, 2025, katika muendelezo wa kampeni za Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza mbele ya wananchi, Ridhiwan Kikwete amebainisha kuwa kupitia uongozi wa Rais Samia, Chalinze imepiga hatua kubwa za kimaendeleo, ikiwemo ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Chalinze yenye majengo 15, iliyogharimu Shilingi Bilioni 7.5, hatua ambayo imesaidia kupunguza changamoto za wananchi kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma za afya.
Aidha, ameeleza kuwa katika kipindi hicho vifo vya kina mama wajawazito vimepungua na kufikia sifuri kutokana na ujenzi wa vituo vya afya na zahanati 23. Pia alibainisha kuwa miradi ya maji imeendelea kutekelezwa ambapo kiwango cha upatikanaji wa maji kimeongezeka kutoka asilimia 52 mwaka jana hadi kufikia asilimia 92, huku ikiahidiwa kufikia asilimia 100 kupitia Ilani ya CCM.
Kwa upande wa elimu, Ridhiwan Kikwete amesema kuwa Chalinze, ambayo zamani ilihusishwa na changamoto za elimu, sasa imepiga hatua kubwa kupitia ujenzi wa shule mpya 17 za msingi na sekondari, mabweni 26 pamoja na nyumba za walimu, hali ambayo imepunguza utoro wa walimu na wanafunzi.
Pia, ameeleza kuwa mapato ya ndani ya Halmashauri ya Chalinze yameongezeka kutoka Shilingi Bilioni 9 mwaka 2021 hadi kufikia Bilioni 22, na sasa bajeti ya Halmashauri hiyo inakaribia Bilioni 41, hatua inayochochea kasi ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Aidha, Ridhiwan Kikwete amewataka wananchi kuendelea kumpa kura za kishindo mgombea urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, ili aendelee kuongoza nchi na kutatua changamoto za wananchi wa Chalinze na Watanzania kwa ujumla.