NA JOHN BUKUKU- DAR ES SALAAM
Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea kuweka msisitizo katika ahadi za kuwaletea Watanzania maendeleo endelevu kupitia sekta za kilimo, elimu, afya, ardhi na miundombinu mikubwa ya kitaifa katika kampeni zake za kuisaka ikulu kwa Miaka mitano ijayo.
Akiwa amehitimisha kwa kishindo kampeni zake katika mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi, Dkt. Samia aliahidi kuwekeza katika teknolojia ili kuongeza ufanisi wa sekta mbalimbali za kimaendeleo, kuboresha sekta ya elimu kwa kuajiri walimu wa kutosha hasa wa sayansi na hisabati, na pia kutekeleza mradi mkubwa wa maji wa Nakonde utakaosaidia Wilaya za Mtwara Vijijini na Nanyamba.
Katika sekta ya kilimo, alisisitiza kuwa Serikali yake itaendeleza ruzuku za pembejeo, ikiwemo salfa kwa wakulima wa korosho, sambamba na kuimarisha kilimo chenye tija. Pia aliahidi kushughulikia migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji kwa kupima na kupanga matumizi ya ardhi, kutoka hekta milioni 3 hadi milioni 6 ifikapo mwaka 2030.
Katika sekta ya afya, Dkt. Samia alisema Serikali yake itaboresha huduma kwa kupeleka vifaa tiba vya kisasa na kuajiri wataalamu wa afya ndani ya siku 100 za kwanza mara baada ya kuingia madarakani.
Vilevile, aliahidi kuendeleza miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay mkoani Ruvuma, reli ya Lindi Kusini, chuo cha uvuvi Kilwa, pamoja na mradi wa gesi asilia (LNG).
Baada ya ahadi hizo, Dkt. Samia anatarajiwa kuendelea na kampeni zake kesho Septemba 28, 2025, kwa kuhutubia wananchi katika mkutano mkubwa Uwanja wa Sabasaba mjini Kibaha, kabla ya kuelekea Chalinze Msata ambako anasubiriwa kwa shauku na wana CCM wa maeneo hayo.