NA JOHN BUKUKU- MTWARA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuunguruma leo mkoani Mtwara katika mkutano mkubwa wa kampeni.
Katika hotuba yake, Dkt. Samia anatarajiwa kuelezea utekelezaji wa ilani ya Uchaguzi ya 2020/ 2025/ na kunadi ilani mpya ya 2025/ 2030 kuhusu utekelezaji wa mradi wa reli ya kisasa ya Mtwara–Mbamba Bay, mradi mkubwa wa kimkakati utakaounganisha ukanda wa kusini na kurahisisha usafirishaji wa mizigo na bidhaa za kilimo, madini pamoja na viwanda.
Aidha, anatarajiwa kugusia miradi mbalimbali ya huduma za kijamii ikiwemo ujenzi na ukarabati wa shule, zahanati, hospitali na miradi ya maji safi na salama ambayo imelenga kuboresha maisha ya wananchi wa Mtwara na mikoa jirani.
Wananchi wa Mtwara wanakaribishwa kwa wingi katika mkutano huo ambapo hamasa imekuwa ikiendelea hapa Mtwara wananchi wakisubiri kumsikiliza kiongozi huyo ambaye pia ataeleza dira ya maendeleo ya miaka mitano ijayo iwapo CCM itaendelea kupewa ridhaa ya kuongoza nchi.