NA JOHN BUKUKU- MTWARA
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali itatumia teknolojia ya akili bandia katika kilimo, utafiti na uzalishaji wa mbegu pamoja na kufundisha wanafunzi, bila kupoteza mila na tamaduni za Kitanzania.
Ameyasema hayo Septemba 26, 2025, katika muendelezo wa kampeni za chama hicho, zilizofanyika katika Viwanja vya Sabasaba mkoani Mtwara.
Aidha, alibainisha kuwa miaka mitano ijayo itakuwa ya matumizi makubwa ya teknolojia za kisasa, ikiwemo tafiti za udongo, mbegu na afya ya udongo kupitia maabara zilizofunguliwa Dodoma na Sokoine, sambamba na kuanzisha vituo vya zana za kilimo vitakavyowasaidia wakulima kwa gharama nafuu.
Dkt. Samia aliongeza kuwa matumizi ya teknolojia katika minada ya korosho yameleta ufanisi, kwani mnunuzi anaweza kushindana kwa bei hata akiwa mbali na mnada, huku taarifa zote zikitolewa papo hapo kwa wakulima kupitia risiti na ujumbe mfupi wa simu.
Pia, alibainisha kuwa teknolojia hiyo itatumika pia kufundishia mashuleni ili vijana wajifunze kuunganishwa na mila na tamaduni za Kitanzania. Aidha, alisema Serikali inataka kizazi kijacho kiwe na maarifa ya kisasa lakini kikiwa kimejikita katika maadili, mila na desturi za taifa.
Aidha, amebainisha kuwa katika kuzalisha korosho, Tanzania inashika nafasi ya pili nyuma ya Ivory Coast, akieleza kuwa jitihada za Serikali kwa kushirikiana na wakulima zimechangia kuongeza uzalishaji siyo tu wa korosho bali pia wa mbaazi na ufuta.
Dkt. Samia aliongeza kuwa uwekezaji mwingine mkubwa ni ongezeko la skimu za umwagiliaji, ambapo sasa zipo sita na miradi mikubwa miwili yenye thamani ya shilingi bilioni 78.6 inayoendelea kujengwa Ndanda, Masasi na Arusha chini Wilaya ya Mtwara.
Aidha, amebainisha kuwa Serikali itaendelea kutafuta masoko ya uhakika kwa mazao yote ikiwemo ufuta na mbaazi, sambamba na kuvutia wawekezaji kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya kuchakata korosho katika kongani ya viwanda kijiji cha Malonje, Wilaya ya Mtwara.
Pia, amesema Serikali itaendelea kusimamia kwa karibu vyama vya ushirika ili kuondoa ubadhirifu na ucheleweshaji wa malipo kwa wakulima. Alibainisha kuwa Benki ya Ushirika iliyoanzishwa inalenga kutoa huduma bora kwa vyama vya ushirika ili kuimarisha kilimo nchini.
Aidha, Dkt. Samia alisema anatambua changamoto ya migogoro kati ya wakulima na wafugaji hususan Nanyumbu, na kueleza kuwa Serikali inaendelea kupima maeneo maalum ya ufugaji kwa ajili ya wafugaji kupitia mpango wa kupeleka ekari milioni 3 hadi milioni 6, huku wakulima wakiendelea na kilimo.
Vilevile, alisema Serikali imewekeza katika huduma za afya ikiwemo kuzindua Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini Mtwara mwaka 2023, ambayo imesogeza huduma za kibingwa kwa wakazi wa mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma.
Aidha, alibainisha kuwa Mkoa wa Mtwara sasa una hospitali mbili za rufaa na hospitali tatu za halmashauri, huku Serikali ikiwa na mpango wa kuongeza watumishi wa afya 5,000 wakiwemo madaktari na wauguzi.
Pia, Dkt. Samia alisema zaidi ya shilingi bilioni 87 zimetolewa kwa ajili ya miradi ya maji na akaahidi kukamilisha mradi wa Makonde pamoja na ule wa kuvuta maji kutoka Mto Ruvuma ili kumaliza changamoto za maji Nanyamba, Mtwara Vijijini na Mtwara Mjini.
Katika sekta ya elimu, alisema Serikali inaendelea kuwekeza katika kuboresha mazingira ya kusomea na kufundishia, kujenga nyumba za walimu na kuongeza vifaa vya kufundishia. Alisisitiza kuwa uwekezaji huo ni kama kupanda mbegu zitakazovunwa baada ya miaka kadhaa kwa vizazi vijavyo.