NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga SC, wameanza kampeni yao ya kutetea taji kwa ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Pamba Jiji FC, katika mchezo wa kwanza uliopigwa leo Septemba 24, 2025, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Katika mchezo huo uliovutia mashabiki wengi, Yanga SC walitawala mchezo na kwenda mapumziko wakiwa kifua mbele kwa bao 1-0, lililofungwa na kiungo chipukizi wa kimataifa kutoka Mali, Lassine Kouma, dakika ya 45+4.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi zaidi, ambapo dakika ya 63, mshambuliaji matata Maxi Mpia Nzengeli aliiongezea Yanga bao la pili.
Wakati mchezo ukielekea ukingoni, kiungo mkongwe Mudathir Yahya alikamilisha karamu ya mabao kwa kufunga bao la tatu dakika ya 90+2, na kuihakikishia Yanga alama zote tatu muhimu.
Kwa ushindi huu, Yanga SC wanaendelea kuonesha dhamira yao ya kutetea ubingwa, huku wakionesha kiwango bora na umakini mkubwa tangu mwanzo wa msimu huu mpya.