NA JOHN BUKUKU- RUANGWA LINDI
Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amepongeza hatua kubwa zilizofikiwa na Jimbo la Ruangwa katika sekta ya michezo, hususan ujenzi wa Uwanja wa Majaliwa ambao amesema ni chachu ya maendeleo ya vijana na kuibua vipaji vipya.
Akizungumza na wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika Septemba 24, 2025 katika Uwanja wa Soko la Madini, Dkt. Samia alisema michezo ni ajira na furaha, kwani inawasaidia vijana kupata fursa za kipato na kujenga mshikamano wa kijamii.
Aidha, alimpongeza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa jitihada zake za kuhakikisha Ruangwa inapata uwanja wa kisasa unaochochea maendeleo ya soka na michezo mingine. Dkt. Samia alibainisha kuwa serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za michezo kwa kushirikiana na wadau ili kuhakikisha vipaji vya vijana vinaibuliwa na kuendelezwa.
Mbali na michezo, alitaja maeneo mengine ya kipaumbele kwa Ruangwa likiwemo afya, elimu, maji, barabara, kilimo na umeme. Amesema kuwa miradi iliyotekelezwa katika miaka iliyopita ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM chini ya usimamizi wa Kassim Majaliwa kama Mbunge wa Ruangwa na Waziri Mkuu wa Tanzania.
Aidha, Dkt. Samia alisema ataendelea kumtumia Majaliwa kama msaidizi wake makini na muhimu serikalini, akimueleza kuwa ni mzalendo na mchapa kazi.
Pia, ameahidi kuendeleza ujenzi wa shule, vituo vya afya, zahanati na miradi ya maji safi na salama, pamoja na kushughulikia changamoto za wanyama waharibifu kwenye mashamba katika maeneo ya Makanjiro, Mandawa, Narungombe, Mbwemkuru na Nambilanje.
Katika sekta ya kilimo, amesema serikali itaendelea kutoa ruzuku za mbolea na pembejeo kwa wakulima, sambamba na kuhakikisha mazao ya biashara na chakula yanapata masoko ya uhakika na bei ya haki.
Pia, Dkt. Samia alisisitiza kuwa kazi za maendeleo bado zipo na serikali itaendelea kushirikiana na wananchi kuhakikisha Ruangwa inaendelea kunufaika na miradi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi.




