Mgombea ubunge jimbo la Arumeru Mashariki ,Joshua Nassari akizungumza na waandishi wa habari kwenye mahafali hayo jijini Arusha.
Meneja wa shule hiyo ,Julius Kimani Macharia akizungumzia kuhusiana na mahafali hayo jijini Arusha.
Mkufunzi Mkuu wa walimu shuleni hapo Aloyce John Shirima akizungumza kwenye mahafali hayo jijini Arusha
…….
Happy Lazaro, Arusha
Arusha .Mgombea ubunge jimbo la Arumeru Mashariki ,Joshua Nassari amewataka wazazi kuendeleza vipaji vya watoto wao badala ya kuwakatisha tamaa ili waweze kufikia malengo yao waliyojiwekea .
Ameyasema hayo jijini Arusha wakati akizungumza katika mahafali ya 5 ambapo jumla ya wanafunzi 42 walihitimu katika shile ya mchepuo wa kiingireza ya Silverleaf Academy iliyopo Usa River wilayani Arumeru mkoani Arusha.
Amesema kuwa, wazazi wengi wamekuwa kikwazo kikubwa cha kuwakatisha tamaa watoto wao kulingana na kile wanachopenda kusomea na mwisho wa siku kuzima ndoto zao jambo ambalo halitakiwi.
“Unakuta mtoto anapenda kuwa daktari na ndoto zake ni kusoma hadi kuwa daktari lakini mwisho wa siku mzazi mwenyewe anamwambia mtoto aachane na hiyo fani au anagoma kumsomesha ambapo hali hii inachangia mtoto kukata tamaa ya kusoma kutokana na mzazi mwenyewe.”amesema Nassari.
Aidha amewataka wazazi kuwa karibu na watoto wao badala ya kuaachia jukumu hilo wasichana wa kazi jambo ambalo hufanya watoto kujiachia kwa kushinda kwenye TV muda wote badala ya kupata muda wa kujisomea .
“Naipongeza shule hii kwa namna ambavyo imekuwa ikiwaandaa wanafunzi kujitegemea kwa kufundisha stadi za kazi tumeona wanafunzi walivyo wabunifu ambapo wanaweza kutengeneza keki,ushonaji,kilimo na hiki ndicho tunachotaka kwa watoto wetu sio elimu ya darasani peke yake kwani hiyo haitoshi ni lazima mtoto ajengewe uwezo zaidi wa kuweza kujitegemea.”amesema Nassari .
Naye Meneja wa shule hiyo ,Julius Kimani Macharia amesema kuwa, shule hiyo imekuwa ikiwaandaa wanafunzi hao kuweza kujiajiri kwa kuwafundisha masomo ya ujasiriamali wakiwa darasa la awali ili kupata uzoefu wakiwa wadogo na kuweza kujitegemea kwa maisha ya baadaye.
“Sisi hapa tumekuwa tukiwaandaa watoto kuanzia elimu ya awali kwa kutoa elimu.kwa vitendo ili wakitoka hapa waweze kujitegemea na hata kuweza kuzalisha ajira na kuwa na ujuzi wa kutosha katika utendaji kazi wao .”amesema .
Amefafanua zaidi kuwa,wao huwa hawatumii viboko kabisa kuna njia mbadala ambayo hutumia katika kuhakikisha wanafunzi wanakuwa na nidhamu katika ufundishaji kwani wana njia bora za ufundishaji ambazo humfanya mwananfunzi aelewe vizuri sana bila kutumia kiboko .
“Shule yetu pia tumekuwa tukifundisha masomo ya ujasiriamali na michezo kuanzia chekechea hadi darasa la saba ambapo wanafunzi wetu wamekuwa wakitumia tablet wakiwa darasani na kuweza kujifunza mambo ya teknolojiabl “amesema .
Kwa upande wake Mkufunzi Mkuu wa walimu shuleni hapo Aloyce John Shirima amesema kuwa ,wanatoa huduma bora kwa wanafunzi na kuhakikisha yupo vizuri kiakili kwa kufuatilia kwa makini maendeleo ya mwanafunzi katika kila somo .
Amesema kuwa, shule hiyo inawekeza zaidi katika mafunzo kwa vitendo ili pindi mwanafunzi anapohitimu anakuwa na ujuzi wa kutosha katika fani mbalimbali na kumwezesha kwenda kutumia ujuzi huo popote atakapokuwa na hata kuweza kuajiri wengine .
“Mitihani sio pekee inayomwezesha mtoto kupata ajira bali tunaamini katika kufundisha kwa vitendo zaidi na kuhakikisha tunahimiza matumizi ya teknolojia pamoja na kazi za mikono na tunahakikisha mwanafunzi yoyote mwenye kipaji analinda kipaji chake kwa kuhakikisha tunakiendeleza kipaji.chake ili.aweze kukifanyia kazi kipaji hicho na kuweza kufikia malengo yake ya baadaye.”amesema .