Na Mwandishi Wetu, Kisarawe
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kitaendelea kulinda amani, umoja na mshikamano kwa kuwa bado hakijakamilisha lengo la kuwatumikia Watanzania na kuwaletea maendeleo makubwa zaidi.
CCM imesema jukumu la kulinda amani umoja, mshikamano na kuleta maendeleo makubwa ya Tanzania imelirithi kutoka kwa vyama vya ukombozi Tanu na Afro Shiraz, hivyo itaendelea kulilinda kwa wivu mkubwa.
Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira alieleza hayo jana, Kisarawe mkoani Pwani alipokuwa akizungumza na viongozi na wanachama wa CCM Mkoa wa Pwani akiwa katika ziara ya kumwombea kura mgombea urais wa CCM Dk. Samia Suluhu Hassan pamoja na wagombea ubunge na udiwani waliosimamishwa na Chama kwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu.
“CCM imekabidhiwa jukumu la kuendeleza umoja, mtu akijaribu kuvunja umoja anavunja msingi tuliokabidhiwa, CCM hatuwezi kuwa miongoni mwa wale wanaounga mkono wanaotaka kuvunja umoja wa nchi, ni kazi tulikabidhiwa, ya historia,” alisema.
Mbali na hlio, alisema kazi ya pili ambayo CCM imekabidhiwa na inaendelea kuisimamia ni kuhakikisha amani inaendelea kudumu.
“Msingi wa amani ni umoja mkivunja umoja amani inakwisha, ndiyo, amani, amani ni kitu muhimu lakini ukikizoea unaweza kuona ni bure kama hewa maana hewa unaihitaji zaidi unapokaribia kufa ndipo unasema leteni mashine tuongeze hewa, lakini hii ya sasa bure tu unafikiri ni sawa inapatikana haina tabu, lakini amani ikitoweka haiwezi kurudi na waliokwisha onja ukosefu wa amani wanajua na msingi mkubwa ni ubaguzi.
“Wanagombana kwa makabila yao, wanagombana kwa dini zao, halafu amani inatoweka, ni matatizo madogo madogo sana lakini gharama yake ni kubwa,” alieleza.