Na Meleka Kulwa -Dodoma
Serikali kupitia Mamlaka ya Uwekezaji wa Maeneo Maalumu ya Kiuchumi (TISEZA) imetoa wito kwa wawekezaji wa ndani na nje kuchangamkia fursa ya kuwekeza katika eneo la Nala, Jijini Dodoma, ambalo limetengwa kwa ajili ya ujenzi wa viwanda mbalimbali,
Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano wa TISEZA, Pendo Gondwe, ameyasema hayo Septemba 23, 2025, Jijini Dodoma, mbele ya waandishi wa habari wakati walipotembelea eneo maalumu la kiuwekezaji.
”Serikali imeweka mazingira rafiki ya uwekezaji ikiwemo kutoa viwanja bure kwa atakayekidhi vigezo na kuanza ujenzi ndani ya mwaka mmoja tangu kupatiwa eneo” amesema Bi. Pendo Gondwe
Aidha,Bi. Pendo Gondwe, amesema kuwa serikali imeondoa kodi kwenye baadhi ya maeneo muhimu kama vile uingizaji wa mitambo ya viwanda na malighafi ili kurahisisha ukuaji wa sekta ya viwanda.
Aidha , amebainisha kuwa dhamira ya mamlaka hiyo ni kuhakikisha Nala inakuwa kitovu cha viwanda ifikapo mwaka 2030, na kampeni ya kuhamasisha uwekezaji inaendelea kutekelezwa.
Kwa upande wake, Meneja wa Kanda ya Kati wa TISEZA, Venance Mashiba, amesema kuwa serikali tayari imewekeza kwenye miundombinu yote muhimu ikiwemo maji, umeme na barabara.
Aidha, amebainisha kuwa mwekezaji wa ndani anatakiwa kuwa na mtaji usiopungua dola bilioni tano na wa nje dola milioni 10, huku kila mmoja akitakiwa kutoa ajira zisizopungua 100, Pia, Mashiba amesema kuwa tangu 12 Agosti mwaka huu walipozindua mpango mkakati huo, wawekezaji wanne wa ndani wamekidhi vigezo .