NA JOHN BUKUKU- NAKAPANYA
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiwa katika mkutano wa kampeni uliofanyika Nakapanya, Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, amewaeleza wananchi kuwa serikali tayari imenunua ndege zisizo na rubani (drone) tano kwa ajili ya kufukuza na kudhibiti wanyama hatarishi hususan tembo wanaovamia makazi na mashamba ya wananchi.
Dkt. Samia alisema hatua hiyo inalenga kulinda usalama wa wananchi pamoja na mali zao, sambamba na kuhakikisha juhudi za wananchi katika kilimo hazipotei kutokana na uharibifu unaosababishwa na wanyamapori.
“Serikali yenu ya CCM haijakaa kimya, tumeshanunua drone tano ambazo zitakuwa zikisaidia kuwafukuza tembo na wanyama wengine wakali pindi wanapovamia makazi na mashamba yenu. Hii ni hatua ya kisasa itakayopunguza tatizo kwa haraka na bila kuathiri maisha ya wananchi,” alisema Dkt. Samia.
Aliongeza kuwa mbali na drone hizo, serikali inaendelea kuimarisha doria za askari wanyamapori na kutoa elimu kwa jamii juu ya namna ya kujilinda na wanyama hao, huku akiwasihi wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya usalama katika kutoa taarifa mapema wanapoona tishio la wanyamapori.
Wananchi wa Nakapanya walilipokea kwa shangwe tangazo hilo, wakisema kuwa ni suluhisho la muda mrefu kwa tatizo lililokuwa likiwakosesha mavuno na kipato.