
Mwenyekiti ws Chama cha Mawakili wa Serikali (Public Bar Association – PBA) Wakili Ado Mwasongwe akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 23, 2025 jijini Dar es Salaam
……………
Chama cha Mawakili wa Serikali (Public Bar Association – PBA) kimetoa tamko rasmi kupinga maazimio ya Chama cha Wanasheria Tanganyika (Tanganyika Law Society – TLS) kuhusu tukio la Septemba 15, 2025, kikisisitiza kuwa maamuzi hayo yanakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sheria za nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Septemba 23, 2025, Mwenyekiti wa PBA, Wakili Ado Mwasongwe, amesema kuwa chama hicho kimeona ni muhimu kutoa ufafanuzi wa kisheria na kikatiba, ili kulinda maslahi ya taifa pamoja na haki za wananchi.
“TLS ni chama cha kitaaluma kilichoanzishwa kwa mujibu wa sheria. Kila wakili aliyeandikishwa ni mwanachama wake, wakiwemo mawakili wa Serikali na hata Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Ni lazima tamko lolote la TLS liwe na weledi wa kisheria, si msukumo wa kiharakati,” amesema Wakili Mwasongwe.
PBA imeonya kuwa hatua ya TLS kuzuia wanachama wake kutoa msaada wa kisheria ni kinyume cha Katiba na Sheria ya Msaada wa Kisheria (Legal Aid Act), na inaleta hatari ya kunyima wananchi maskini haki yao ya msingi ya kupata huduma hiyo.
“Huduma za msaada wa kisheria siyo hiari wala hisani. Ni jukumu la kisheria kwa mujibu wa Sheria ya Msaada wa Kisheria, na kila wakili anawajibika kutoa huduma hiyo kwa wote — wenye uwezo na wasio na uwezo,” amesema
Amefafanua kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasisitiza juu ya usawa mbele ya sheria (Ibara ya 13) pamoja na wajibu wa kila mtu kutii Katiba na sheria (Ibara ya 26).
“Hatua ya TLS ya kuwanyima wananchi wa kipato cha chini msaada wa kisheria ni kitendo cha kibaguzi na kinyume cha Katiba,” amesema Wakili Mwasongwe.
Katika maelezo yake, Wakili Mwasongwe amewakumbusha viongozi wa TLS kuwa masuala ya nidhamu ya mawakili yako chini ya Kamati ya Nidhamu ya Mawakili, inayoongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu, hivyo si jukumu la TLS peke yake kuyasimamia.
“Tunashauri kwa heshima kuwa viongozi wa TLS wazingatie wajibu wao wa kisheria na kitaaluma, na waache mara moja kuchagua sheria za kutii kulingana na maslahi yao binafsi. Wanapaswa kutii sheria zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesisitiza
PBA imesisitiza kuwa itaendelea kutetea misingi ya utawala wa sheria, kulinda maslahi ya taifa, na kuhakikisha kuwa wananchi wote hususan wale wa kipato cha chini wanapata huduma za kisheria bila ubaguzi wa aina yoyote.