Kaimu Mkurugenzi wa Michezo Jeshini, Luteni Kanali Penina Igwe akizungumza katika mapokezi maalum mwanariadha Alphonce Felix Simbu, ambaye ametwaa medali ya dhahabu katika mashindano ya dunia ya mbio za marathoni kwa wanaume yaliyofanyika Tokyo, Japan, yaliyofanyika leo Septemba 23, 2025 alfajiri katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Mwanariadha Alphonce Felix Simbu, akizungumza na waandishi wa habari katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

Picha za matukio mbalimbali wakati wa mapokezi ya Mwanariadha Alphonce Felix Simbu, ambaye ametwaa medali ya dhahabu katika mashindano ya dunia ya mbio za marathoni kwa wanaume yaliyofanyika Tokyo, Japan.
……..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limesema litaendelea kufanya uwekezaji katika sekta ya michezo kwa lengo la kulea vipaji, pamoja na kufuata sera, miongozo na mipango, huku wakimpongeza mwanariadha wao, Alphonce Felix Simbu, ambaye ametwaa medali ya dhahabu katika mashindano ya dunia ya mbio za marathoni kwa wanaume yaliyofanyika Tokyo, Japan.
Akizungumza katika mapokezi maalum yaliyofanyika leo Septemba 23, 2025 alfajiri katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Michezo Jeshini, Luteni Kanali Penina Igwe, amesema wanajivunia mafanikio ya Simbu na itaendelea kutoa kipaumbele kwa michezo kama sehemu ya mkakati wa maendeleo ya vipaji vya vijana.
“Tunajivunia kwa kutunza na kulea vipaji kama Simbu. Hii ni ishara kwamba tuna hazina kubwa ya vijana wenye vipaji. Tunaamini tutazidi kufanya vizuri, hasa kwenye mchezo wa riadha,” amesema Luteni Kanali Igwe.
Aidha, amebainisha kuwa ushindi wa Simbu ni wa kihistoria kwa sababu ni mara ya kwanza kwa Mtanzania kutwaa medali ya dhahabu katika mashindano makubwa ya kimataifa ya mbio za marathoni.
“Katika michezo ya kiushindani, lazima tujiimarishe kwa kuwa na wataalam waliobobea, kuwapeleka kwenye mafunzo ya mara kwa mara, na kuimarisha miundombinu ya kisasa. Tunaamini tunaweza kufanya zaidi ya haya,” amengeza Luteni Kanali Igwe.
Amesema kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano wa karibu kati ya JWTZ, Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), ambao umewasaidia wanamichezo kushiriki katika mashindano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.
Kwa upande wake, Alphonce Simbu, amesema kuwa siri ya mafanikio yake ni nidhamu, kujituma na ushirikiano mzuri na wenzake katika kipindi chote cha mazoezi.
“Tumekuwa tukishirikiana kwa karibu na wachezaji wenzangu. Ushindi huu nimeufanikisha baada ya juhudi za miaka 10. Nilishiriki kwa mara ya kwanza mwaka 2015 nchini China, mwaka 2017 nikashika nafasi ya tatu huko London, lakini sikukata tamaa hadi mwaka huu nilipofanikiwa kutwaa dhahabu,” amesema Simbu.
Amewatia moyo wanamichezo nchini kuongeza juhudi na nidhamu, huku akisema kila mchezaji ana uwezo wa kufanya vizuri endapo atazingatia misingi hiyo.
Katika mapokezi hayo, viongozi mbalimbali wa Serikali, Jeshi na Sekta ya michezo wamehudhuria mapokezi hayo pamoja na wanariadha wenzake, ambao walimpongeza kwa kazi kubwa aliyofanya na kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania.
Septemba 15, 2025, Alphonce Felix Simbu ameweka historia kwa kuwa Mtanzania wa kwanza kutwaa medali ya dhahabu katika mashindano ya dunia ya riadha, na hivyo kuiandikia Tanzania ukurasa mpya katika tasnia ya michezo ya kimataifa.





