NA JOHN BUKUKU- RUVUMA
Mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuufanya mkoa wa Ruvuma kuwa ukanda mkubwa wa biashara sambamba na kuwa kitovu cha usalama wa chakula nchini na katika nchi jirani.
Akizungumza Septemba 22, 2025 katika mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja wa VETA Msamala mjini Songea, Dkt. Samia alisema mkoa wa Ruvuma umechangia kwa kiasi kikubwa katika suala la usalama wa chakula, hususan kupitia zao la mahindi na kahawa, na hivyo umeendelea kuwa nguzo ya taifa katika sekta ya kilimo.
“Tumejenga jumla ya maghala 28 ya kuhifadhia mazao mkoani Ruvuma, ikiwa ni sehemu ya kuhakikisha wakulima wanalinda mazao yao na taifa linajipatia uhakika wa chakula,” alisema Dkt. Samia. Alifafanua kuwa kati ya hayo, Halmashauri ya Wilaya ya Songea ina maghala 11, Madaba maghala 9, Namtumbo maghala 7, na Nachingwea ghala 1.
Aidha, alieleza kuwa ruzuku za mbolea na pembejeo zimelenga kuongeza tija ya kilimo, huku akiwataka wakulima kuzitumia kwa ajili ya mashamba yao badala ya kuziuza. “Ruvuma ni nyumbani kwa kilimo, ndiyo maana tunajielekeza zaidi katika kuongeza thamani kupitia viwanda vya kuchakata mazao ili vijana wengi wapate ajira,” aliongeza.
Akigusia sekta ya kahawa, Dkt. Samia alisema uzalishaji umeongezeka kutoka tani 1,980 hadi 3,052 na akatoa ahadi ya kuweka mitambo ya kisasa ya kukoboa kahawa kabla ya kuuzwa ili kuongeza thamani na kipato kwa wakulima.
Mbali na kilimo, alieleza miradi mbalimbali ya miundombinu inayoendelea ikiwemo ukarabati wa kiwanja cha ndege cha Songea, ujenzi wa bandari ya Mbamba Bay unaoendelea kwa asilimia 35, na mradi wa reli ya kisasa ya kilometa 1,000 inayounganisha Mtwara na Ruvuma.
“Kwa uwekezaji huu mkubwa, Ruvuma inakwenda kuwa ukanda wa biashara wa kimkakati. Tutahakikisha mawasiliano, miundombinu ya usafiri wa anga, barabara na maji yanaboreshwa ili wafanyabiashara watumie njia zote kufanikisha biashara zao,” alisema.
Kwa upande wake, mgombea mwenza Emmanuel Nchimbi aliwapongeza wananchi wa Ruvuma kwa mwitikio mkubwa na kusisitiza kuwa miradi mikubwa iliyotekelezwa na Dkt. Samia imejenga imani kubwa ya wananchi kwa CCM.
Alitoa wito kwa Watanzania kuhakikisha wanatunza vitambulisho vya kupiga kura na kujitokeza kwa wingi Oktoba 29 ili kumchagua Dkt. Samia pamoja na wagombea wote wa CCM.