Na Jeston Kihwelo, WANMM, Dodoma
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kuajiriwa watumishi wapya 312 katika sekta ya Ardhi hatua itakayoongeza ufanisi katika utoji huduma katika sekta Ardhi nchini.
Mhandisi Sanga ametoa shukurani hizo mwishoni mwa wiki wakati wa mafunzo ya awali kwa watumishi wapya 126 wa kada za Upimaji Ardhi na Mafundi Sanifu ambao ni sehemu ya waajiriwa wapya 312 yaliyofanyika Makao Makuu ya Wizara hiyo katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
“Tunamshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuamini na kutuwezesha kupata watumishi wapya. Huu ni uwekezaji mkubwa kwa taifa katika kuhakikisha huduma za ardhi zinaboreshwa kwa vitendo” alisema Katibu Mkuu Mhandisi Sanga.
Akizungumza na watumishi hao wapya, Mhandisi Sanga amewahimiza kufanya kazi kwa nidhamu, weledi na kushirikiana kwa karibu na viongozi wao wa kazi, watumishi wengine watakaowakuta kwenye vituo vya kazi walivyopangiwa pamoja na wananchi watakaofika kupata huduma za ardhi.
Aidha, amewasihi watumishi hao kuwa na tabia ya kuweka akiba, kuachana na tamaa ya fedha za haraka, na kuitii serikali yao, kutujituma, kuwa na ushirikiano, na kufanya kazi kwa moyo wa kizalendo.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi. Lucy Kabyemera aliwataka Mafundi Sanifu na Wapima Ardhi walioajiriwa kuhakikisha wanazingatia afya zao ili wakutoe huduma kwa ubora wa juu ili kufikia malengo ya serikali.
“Afya ni msingi wa utendaji bora. Jiungeni na huduma za bima, fanyeni mazoezi, jilindeni na magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza. Kazi yenu inahitaji nguvu, akili na umakini hivyo lindeni miili yenu,” alisema Bi. Lucy Kabyemera.
Ujio wa watumishi wapya katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ni sehemu ya juhudi za serikali za Awamu ya Sita katika kuongeza rasilimali watu ili kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.