Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kujenga Reli ya Kisasa kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay, Wilaya ya Nyasa, hatua itakayochochea shughuli mbalimbali za kiuchumi katika eneo hilo.
Akizungumza leo, Septemba 21, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika Mbamba Bay, Nyasa, Rais Dkt. Samia amesema kuwa tayari mazungumzo yanaendelea kufanikisha utekelezaji wa mradi huo mkubwa wa Reli ya Kisasa, unaotarajiwa kuleta tija kubwa kwa uchumi wa wananchi.
Katika sekta ya afya, Rais Dkt. Samia amesema Serikali imeendelea kuboresha huduma kwa kujenga Hospitali ya Wilaya, vituo vya afya, pamoja na ujenzi wa zahanati tisa (9) katika Wilaya ya Nyasa.
“Tumeajiri watumishi 316 katika sekta ya afya hapa wilayani. Ikiwa mtanipa ridhaa ya kuendelea kuongoza tena, tunatarajia kuajiri watumishi 5,000 katika sekta ya afya,” amesema Dkt. Samia.
Ameongeza kuwa katika sekta ya elimu, Serikali imefanikiwa kujenga shule 12, sita kati ya hizo ni shule za msingi na sita ni shule za sekondari, pamoja na kuanzisha Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) katika wilaya hiyo.
Kuhusu sekta ya nishati, Rais Samia amesema Serikali inapanga kujenga kituo cha kupozea umeme kutoka Songea hadi Nyasa, jambo litakalosaidia kutatua changamoto ya upungufu wa umeme na kuvutia wawekezaji katika wilaya hiyo.
Aidha, amesema kuwa Serikali inatarajia kuongeza bajeti ya mikopo kwa wananchi kutoka shilingi milioni 57 hadi kufikia shilingi milioni 345, ili kuwawezesha wananchi zaidi kiuchumi.
Vilevile, Rais Dkt. Samia amesema Serikali inaendelea kujenga na kuboresha miundombinu ya barabara katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo, ili kuimarisha usafiri na uchukuzi.