NA JOHN BUKUKU- MBINGA
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewapongeza wananchi wa wilaya ya Mbinga kwa mshikamano na mapokezi makubwa, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni ishara ya upendo na imani kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza Septemba 21, 2025, katika muendelezo wa kampeni za CCM wilayani humo, Dkt. Samia alisema serikali itaendelea kuimarisha sekta ya afya na elimu kwa kujenga shule na hospitali zaidi, kuongeza upatikanaji wa dawa na vifaa tiba, pamoja na kuboresha huduma za matibabu kwa wananchi wa Mbinga.
Vilevile, aliwapongeza wakulima wa wilaya hiyo kwa jitihada zao katika kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara, huku akiahidi kuwa serikali itaendeleza ruzuku za pembejeo, mbolea na huduma za ugani kupitia programu maalum za vijana.
Aidha, alisema serikali itaendelea kutafuta masoko na kuhakikisha bei nzuri ya mazao ili wakulima wa Mbinga na Tanzania kwa ujumla wanufaike na jasho lao, sambamba na kuendeleza barabara kuu na za miji zilizotajwa kuwa miongoni mwa vipaumbele vya awamu ijayo.
Dkt. Samia alibainisha pia kuwa Mbinga ni sehemu yenye historia kubwa kwa taifa, ikiwemo kuwa eneo alikosoma Rais wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Benjamin William Mkapa, katika Shule ya Sekondari ya Kigonsera, sambamba na kuwa kitovu cha uzalishaji wa mazao ya kilimo.
Akifafanua utekelezaji wa miradi, alisema serikali yake imetekeleza miradi mingi ya maendeleo katika sekta za umeme na maji, ambapo zaidi ya nusu ya vitongoji nchini tayari vimeunganishwa na huduma ya umeme, huku miradi mikubwa ya maji ikiendelea kutekelezwa Mbinga na maeneo mengine.
“Katika vijiji tumefikia nusu, sasa tupo kwenye vitongoji. Miaka mitano ijayo tutamaliza vitongoji vilivyosalia ili kila Mtanzania afikishiwe huduma ya umeme,” alisema Dkt. Samia.
Aidha, aliongeza kuwa serikali imetoa shilingi bilioni 4.6 kwa ajili ya mradi mkubwa wa maji utakao hudumia kata nane zilizobaki mjini Mbinga, huku akiahidi miradi mingine kuendelea kusogezwa karibu ili kila kaya ipate huduma hiyo muhimu.




