Mgombea Mwenza wa Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Emmanuel John Nchimbi, amempongeza Mgombea wa Urais wa chama hicho, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uwezo wake mkubwa wa kutafuta rasilimali, kusimamia mgawanyo wake, pamoja na kuleta maendeleo jambo linalowafanya CCM kutembea kifua mbele katika kipindi hiki cha uchaguzi.
Akizungumza leo, Septemba 21, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika Mbamba Bay, Wilaya ya Nyasa, mkoani Ruvuma, Dkt. Nchimbi wakati akitoa salamu kwa Rais Dkt. Samia, amesema kuwa katika mikoa 11 aliyofanya kampeni, wananchi wameahidi kumpigia kura Rais Samia na chama chake kwa kishindo kikubwa.
“Mikoa yote 11 wamenituma nikwambie, Mheshimiwa Rais Dkt. Samia, kuwa utashinda kwa kishindo. Kuanzia kwa Madiwani wetu wote wa CCM, watashinda,” amesema Dkt. Nchimbi.
Aidha, amemshukuru Rais Samia kwa kumuamini na kumpendekeza kuwa Mgombea Mwenza wa Urais, na ameahidi kushirikiana naye kikamilifu katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali kwa lengo la kufanikisha malengo ya kuwahudumia Watanzania.
Dkt. Nchimbi ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura mwezi Oktoba mwaka huu.