NA JOHN BUKUKU
Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewatoa hofu Watanzania na kuonya vikali wale wote wanaopanga kuleta vurugu kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Akihutubia wakazi wa Pemba kwenye mkutano wa kampeniuliofanyika Gonbani ya Kale, tarehe 20 Septemba 2025, Rais Dkt. Samia alisema kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha uchaguzi unafanyika katika hali ya amani, huku akiwahimiza wananchi wasikubali kuchokozeka na wachache wenye nia ya kuharibu utulivu wa taifa.
“Amani ni tunu muhimu sana kwa Taifa letu. Hakikisheni mnaepuka kuchokozeka au kushiriki katika vitendo vinavyoweza kuhatarisha utulivu wa nchi. Wale wote wanaopanga vurugu wajue kuwa hawatapata nafasi,” alisema Dkt. Samia.
Amesisitiza kuwa uchaguzi mkuu utakuwa wa haki, huru na utakaosimamiwa kwa misingi ya kidemokrasia, hivyo wananchi wanapaswa kujitokeza kwa wingi kupiga kura bila woga wala mashaka.
“Niwatoe hofu. Hakutakuwa na vurugu. Nendeni mkapige kura kwa amani ili kuchagua viongozi mnaowataka,” aliongeza Rais Samia.
Kauli hiyo imelenga kuwatia moyo wananchi kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi huku wakizingatia mshikamano wa kitaifa na kulinda utulivu wa nchi.