NA JOHN BUKUKU
Mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema serikali ya chama hicho imepanga kufungua Kisiwa cha Pemba kiuchumi kupitia miradi mikubwa ya maendeleo itakayochochea shughuli za kiuchumi na biashara. Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Pemba, Bandari ya Wete na zaidi ya barabara saba ikiwemo ile ya kutoka Chake Chake kwenda Mkoani.
Wakazi wa Kisiwa cha Pemba walifurika Gombani ya Kale kumlaki na kumsikiliza Mgombea Urais kupitia CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akinadi Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho kwa mwaka 2025-2030.
Dkt. Samia amesema serikali ya CCM imedhamiria kukuza uchumi wa Pemba kwa kuanzisha miradi muhimu ikiwemo barabara za lami ndani ya kisiwa hicho, pamoja na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Pemba.
“Serikali ya CCM itahakikisha miradi hii inatekelezwa kwa ufanisi ili kufungua fursa mpya za ajira, uwekezaji na biashara kwa wananchi wa Pemba,” alisema Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Wakati huohuo, Dkt. Samia ametumia nafasi hiyo kuwatoa hofu Watanzania kuwa siku ya uchaguzi Oktoba 29 hakutakuwa na vurugu za aina yoyote, na amewataka kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwani vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kikamilifu kulinda amani na utulivu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Hemed Suleiman Abdullah, naye alitumia mkutano huo kumpigia debe Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Dkt. Hussein Ally Mwinyi, akisisitiza kuwa kwa kazi kubwa zilizofanywa miaka mitano iliyopita, viongozi hao wanastahili kupewa miaka mingine mitano.
Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Asha-Rose Migiro, aliwaombea kura wagombea wote wa CCM, huku Prof. Makame Mbarawa, Mgombea Ubunge wa Jimbo la Mkoani kupitia CCM, akiungana na wananchi kuhakikisha utekelezaji wa Ilani unaimarisha zaidi uchumi wa Pemba.
Baada ya kishindo cha Dkt. Samia Suluhu Hassan Unguja na Pemba, kituo kinachofuata ni Mkoa wa Ruvuma ambako ataendelea na kampeni za kuomba kura ili achaguliwe tena kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi cha pili.