NA JOHN BUKUKU – PEMBA
Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuunguruma kesho katika mkutano mkubwa wa kampeni utakaofanyika Uwanja wa Gombani ya Kale, kisiwani Pemba.
Mkutano huo unatarajiwa kuvutia maelfu ya wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Pemba wakiwa na hamasa ya kumsikiliza mgombea huyo akinadi Ilani ya Uchaguzi ya CCM pamoja na ahadi za maendeleo zinazolenga kuendeleza kasi ya ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kamati ya kampeni ya CCM Zanzibar, maandalizi yote muhimu yamekamilika, ambapo viongozi wa chama hicho pamoja na wagombea wa ngazi mbalimbali wataungana na Rais Samia kunadi sera za CCM na kueleza utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020/2025 pamoja na dira mpya ya maendeleo kupitia Ilani ya 2025/2030.
Aidha, mkutano huo utakuwa fursa kwa Dkt. Samia kueleza mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita, ikiwemo miradi ya miundombinu, afya, elimu, nishati na huduma za kijamii, sambamba na kueleza dira ya miaka mitano ijayo.
Viongozi wa CCM Zanzibar wametoa wito kwa wananchi wa Pemba kujitokeza kwa wingi kushiriki mkutano huo, si tu kumsikiliza Dkt. Samia, bali pia kudhihirisha mshikamano na kuonyesha kuwa Pemba ni ngome ya amani na mshikikiano wa kitaifa.
Mkutano wa Gombani unakuja ikiwa ni mwendelezo wa mikutano ya kampeni inayoendelea kote nchini, ambapo Dkt. Samia amekuwa akihimiza Watanzania wote kulinda amani, mshikamano na tunu kuu za taifa katika kipindi chote cha uchaguzi.



