NA JOHN BUKUKU- NUNGWI
Wananchi wa Nungwi, mkoa wa Kaskazini Unguja, wamejitokeza kwa wingi kwenye mkutano wa kampeni wa mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, unaofanyika eneo la Hamburu Nungwi, wilaya ya Kaskazini A Unguja.
Mmoja wa wananchi hao, Mohamed Mwinyi, amesema kuwa atakuwa tayari wakati wote kwenda kupiga kura na atawapigia viongozi wote wa CCM.
“Nawashauri wazee wenzangu wote wakapigie viongozi wote wa CCM na nawashawishi wakapigie Chama Cha Mapinduzi kutokana na amani, utulivu na maendeleo yaliyopatikana katika nchi yetu,” amesema.
Akizungumzia kuhusiana na mapokezi ya Rais Samia, amesema kuwa wamefurahia sana ujio wa Rais Samia na wanamuahidi kumpa mitano tena.
Naye mwananchi mwingine, Dulayo, amesema kuwa mapokezi yapo vizuri sana na wananchi wamejitokeza kwa wingi kumpokea mgombea urais hapa Nungwi.
Amesema kuwa, endapo Dkt. Mwinyi na Rais Samia watapata tena ridhaa ya kuongoza, wameombwa kipaumbele kiwe utengenezaji wa miundombinu ya barabara na shule, kwani magari barabarani yamekuwa mengi na barabara zimekuwa nyembamba, hivyo zinatakiwa kupanuliwa ili zipitike kwa urahisi zaidi.
“Kama tulivyoambizana kuja kwenye mkutano kwa wingi kumsikiliza Rais Samia, ndivyo hivyo hivyo tutaambizana kwenda kwa wingi kupiga kura Oktoba 29, na wawe wengi katika kupiga kura na sio kukurupuka,” amesema.