Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah (katikati) akipiga makofi wakati akizindua Maadhimisho ya Miaka 50 ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) katika hafla iliyofanyika katika Ofisi za TBS leo Septemba 18, 2025 jijini Dar es Salaam (PICHA NA NOEL RUKANUGA)
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah akizungumza wakati akizindua Maadhimisho ya Miaka 50 ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) katika hafla iliyofanyika katika Ofisi za TBS leo Septemba 18, 2025 jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Ashura Katunzi akizungumza wakati uzinduzi Maadhimisho ya Miaka 50 ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) katika hafla iliyofanyika katika Ofisi za TBS leo Septemba 18, 2025 jijini Dar es Salaam
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa TBS, Bw. Hussein Ally akizungumza wakati uzinduzi Maadhimisho ya Miaka 50 ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) katika hafla iliyofanyika katika Ofisi za TBS leo Septemba 18, 2025 jijini Dar es Salaam
…….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah, amezindua maadhimisho ya miaka 50 ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS), huku akielekeza menejimenti ya shirika hilo kutumia maadhimisho hayo kama fursa ya kutangaza uwezo na huduma zinazotolewa na TBS.
Akizungumza leo, Septemba 18, 2025, jijini Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi wa maadhimisho hayo yatakayofikia kilele chake mwezi Desemba 2025, Dkt. Abdallah amesema kuwa maadhimisho hayo ni fursa ya kipekee ya kutafakari miaka 50 ya uhai wa taasisi hiyo muhimu, ambayo imekuwa nguzo ya maendeleo ya viwanda na ustawi wa biashara nchini kwa kulinda afya na ustawi wa jamii kupitia uendelezaji wa viwango pamoja na uthibiti ubora.
Ameeleza kuwa shirika hilo limekuwa muhimili mkubwa katika kuhakikisha bidhaa na huduma zinazopatikana nchini zinakidhi matakwa na viwango vinavyokubalika kitaifa na kimataifa.
“TBS imepiga hatua kubwa, ikiwemo kupanua wigo wa utoaji huduma na kuwa karibu na wananchi pamoja na wadau, hali iliyochangia kuboresha huduma za kielektroniki pamoja na kuimarisha ofisi za kanda,” amesema Dkt. Abdallah.
Amefafanua kuwa shirika hilo limeendelea kuwezesha biashara na kukuza matumizi ya viwango, kanuni za ubora, pamoja na usalama katika viwanda, biashara na huduma mbalimbali.
Ameongeza kuwa viwango vya ubora vina mchango mkubwa katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kuijenga Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kipato cha kati cha juu unaotegemea viwanda.
Akizungumza kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi wa TBS, Bw. Hussein Ally amesema kuwa maadhimisho hayo ni fursa ya kujitathmini na kupanga mikakati bora kwa miaka ijayo kwa kushirikiana na sekta binafsi pamoja na wadau mbalimbali ili kuimarisha sekta ya viwango nchini.
Bw. Ally amesema Taifa linahitaji bidhaa na huduma zinazokidhi viwango vinavyokubalika ili kulinda walaji, kukuza ushindani na kuwezesha bidhaa za Tanzania kuingia katika soko la kimataifa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Ashura Katunzi, amebainisha kuwa hadi sasa, TBS ina jumla ya maabara 12 zilizopata ithibati ya umahiri na vyeti vya kimataifa, hatua inayomaanisha kuwa majibu yanayotolewa na maabara hizo yanatambulika kimataifa.
Amesema maabara hizo zimewekewa mashine za kisasa (state-of-the-art equipment), zenye uwezo wa kutoa matokeo kwa usahihi na kwa wakati sahihi.
Baadhi ya mashine hizo za kisasa ni pamoja na Hydrostatic Pressure Test Machine – inayotumika kupima mabomba ya maji, yenye uwezo wa kupima mabomba yenye kipenyo cha kuanzia inchi 0.5 (mm 12) hadi inchi 32 (mm 800), na uwezo wa kupima hadi sampuli 120 kwa wakati mmoja. Mashine hii inapatikana katika nchi tano pekee barani Afrika, ikiwemo Tanzania.
Mashine nyengine ni Automatic Conductor Resistance Tester – inayopima waya (cables) za umeme wa aina zote, zenye kipenyo hadi milimita 40 au milimita za mraba 1,200.
Pia Solar Simulator – inayotumika kupima ubora wa paneli za sola bila kutegemea mwanga wa jua. Katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, mashine hii inapatikana Tanzania pekee, katika ofisi za TBS.
Maadhimisho ya miaka 50 ya TBS yamebebwa na kaulimbiu isemayo : Kuchochea Ubora na Usalama kwa Maisha Bora.