NA JOHN BUKUKU- NUNGWI, ZANZIBAR
Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea na kampeni zake Septemba 18, 2025, katika uwanja wa Amburu, Nungwi wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja, Zanzibar.
Akizungumza na wakazi wa mkoa huo, Dkt. Samia amesema kuwa katika kunyanyua hali za maisha ya wananchi, Mradi wa TASAF umetekelezwa kwa mafanikio makubwa na umechangia watu wengi kujikwamua kiuchumi pamoja na kusaidia familia zisizojiweza kusomesha watoto.
Aidha, amebainisha kuwa Tanzania ipo vizuri katika masuala ya diplomasia, ulinzi na usalama, na mafanikio hayo yametokana na kulinda na kuenzi Muungano.
“Ndugu zangu Watanzania, tuendelee kuuenzi na kuulinda Muungano wetu, kwa sababu ndiyo umekuwa msingi wa amani, umoja, mshikamano, maendeleo na ustawi wa Taifa letu,” amesema.
Dkt. Samia ameongeza kuwa kwa miaka mitano ijayo, serikali ya CCM itaendelea kukuza uchumi, kuongeza kipato cha wananchi, kuimarisha ustawi wa jamii, kulinda amani, usalama na utulivu, pamoja na kudumisha demokrasia na utawala bora.
Amesema, ili kujenga Taifa linalojitegemea, ni lazima kila mtu au kijana nchini awe na shughuli inayomuingizia kipato. Ameeleza kuwa serikali inaendelea kuandaa mazingira kwa vijana kuweza kuwa na shughuli za kuwaingizia kipato, ili kila mmoja ainue ustawi wa maisha yake.
Dkt. Samia pia amebainisha kuwa Ilani ya CCM ya mwaka 2020–2025 imetekelezwa kwa asilimia mia moja Zanzibar, chini ya uongozi wa Dkt. Hussein Mwinyi, hususan katika uboreshaji wa miundombinu na kukuza uchumi wa bluu.
Aidha, amempongeza Dkt. Mwinyi kwa ushirikiano katika kukuza sekta ya utalii, akibainisha kuwa watalii zaidi ya milioni 5 wamefika Tanzania Bara na zaidi ya laki 7 Zanzibar, hali iliyopelekea kuongezeka kwa mapato ya serikali na ya wananchi.
“Eneo lingine ambalo tumeendelea kulifanyia kazi ni uchumi wa bluu. Tumelifanyia kazi vizuri na tunakwenda kuendelea kulifanyia kazi, hususani kwenye uvuvi wa bahari kuu. Hili ni eneo la Muungano, tunakwenda kulifanyia kazi kwa pamoja,” amesema Dkt. Samia.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar na Mgombea Urais wa CCM Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi, amewataka wananchi kuendelea kudumisha amani, mshikamano na maridhiano.
Aidha, amesema kuwa hakuna maendeleo bila amani, na amewaomba wananchi na wanachama wa CCM kujitokeza kwa wingi ifikapo Oktoba 29 kupiga kura.
Awali, Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Asha-Rose Migiro, amesema kuwa viongozi hao wawili wamesimama kidete kudumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, huku malengo yao yakiwa ni kuendeleza maendeleo ya Tanzania Bara na Zanzibar Visiwani.
Dkt. Migiro pia amebainisha kuwa filamu ya The Royal Tour iliyofanywa na Dkt. Samia imechangia kuongeza idadi ya watalii na kuitangaza Tanzania kimataifa. Aidha, amesifu juhudi za Dkt. Mwinyi katika kujenga miundombinu ya elimu, barabara na vituo vya afya, hatua zilizompa jina la utani la “Hussein Mabati” kutokana na maendeleo aliyoyafanya.