Na Silivia Amandius
Muleba, Kagera.
Wananchi wa Kata ya Kamachumu, wilayani Muleba, wamehimizwa kuendelea kuiamini Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kukipigia kura katika uchaguzi ujao, kutokana na utekelezaji mkubwa wa miradi ya maendeleo uliofanywa katika awamu ya sita ya Serikali.
Kauli hiyo imetolewa na Mgombea Ubunge wa Jimbo la Muleba Kaskazini, Ndugu Adonis Bitegeko, wakati wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi uliofanyika katika kata hiyo.
Bitegeko amesema CCM imefanya mageuzi makubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, kwa kuboresha huduma za matibabu, na elimu, kwa kujenga na kuboresha miundombinu ya kujifunzia. Amesisitiza kuwa maendeleo hayo yanahitaji kuendelezwa kwa wananchi kuichagua CCM kuanzia ngazi ya Urais, Ubunge hadi Udiwani.
Kwa upande wake, Mgombea Udiwani wa kata ya Kamachumu kupitia CCM, Ndugu Leodgad Chonde, ameahidi kushirikiana kwa karibu na Mbunge iwapo atachaguliwa ili kuhakikisha miradi iliyobaki inakamilika kwa wakati, kwa manufaa ya wananchi wote.