Na MWANDISHI WETU, Makete
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira, amesema uamuzi wa kumchagua Mgombea Urais wa CCM, Dk. Samia Suluhu Hassan awanie kiti hicho siyo kumpa zawadi bali ni kutokana na uwezo aliouonesha kuiongoza nchi kwa mafanikio katika kipindi cha miaka minne na nusu.
Amesema Dk. Samia licha ya kuichukua nchi katika mazingira magumu, lakini aliivusha salama na maendeleo makubwa yameshuhudiwa chini ya uongozi wake.
Wasira ameyaeleza hayo jana alipokuwa akizungumza na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Makete mkoani Njombe, kumnadi na kumwombea kura Dk. Samia na kuweka mikakati ya ushindi kwa wagombea wote waliosimamishwa na Chama.
“Hatumpi zawadi, tunamwongeza muda wa kazi kwa sababu kazi yenyewe anaiweza, tunampa kazi anayoiweza, anayoijua. Kwa mfano umenunua gari jipya au ulikuwa nalo, lina dereva anaejua kazi yake uende uazime dereva wa muda halafu akiangusha tutapata wapi gari jingine, unampa dereva anayejua, mwenye leseni.
“Mamlaka haya ni leseni kwamba tulipewa leseni ya kuongoza Tanzania kwa miaka mitano tangu mwaka 2020, ikifika Oktoba 29, 2025 tutawaomba Watanzania ‘kurenew’ leseni yetu, sasa sifa moja ya “kurenew’ leseni yetu ni kuwa na dereva mzuri, sasa kwa nini tuweke dereva mpya aje aangushe gari letu,” alieleza.
Ameeleza kuwa, Dk. Samia amefanya kazi yake vizuri kwa kipindi cha miaka mitano ndiyo maana mwaka huu atamchaguliwa tena katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, kwa kuridhishwa na uongozi wake.