MAKAMU Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira amesema Chama kinaingia katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 huku kikiwa kifua mbele kwa kutekeleza ahadi kilichoahidi kwa wananchi.
Wasira amesema hayo leo Septemba 17, 2025 alipokuwa akizungumza na viongozi wa CCM kutoka majimbo ya Uyole na Mbey Mjini kumwombea kura mgombea urais wa CCM Dk. Samia Suluhu Hassan, wabunge na madiwani waliosimamishwa na CCM kupeperusha bendera katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
“Tunaenda kwenye uchaguzi, moja ya mambo ambayo yanatupeleka kifua mbele ni kwamba tumeahidi na tunatekeleza tena tunatekeleza mambo yanayohusu maisha ya watu.
“Yako mambo mengi, elimu tumekubaliana tubadili mfumo wa elimu, ili kijana akienda ‘secondary school’ akitoka anajua ujuzi wa kazi, tumeeneza umeme, tunapeleka maji, ukiwa na maji ya bomba, bomba likiharibika unafanyaje lazima uwe na watu hapo mtaani kwako ambao wanaweza kurekebisha bomba na ndiyo kazi yao ambayo watakuwa wamesoma.
“Kama umeme unaleta matatizo lazima wawepo vijana wanajua umeme wanaweza kurekebisha umeme unawalipa ndiyo kazi yao wamejiajiri,” amesema Wasira.
Amesema sasa nchini kuna vyuo vikuu 50 ambavyo vinazalisha wahitimu wengi kila mwaka hivyo kusababisha upatikanaji wa ajira kuwa changamoto.
“Tuna universities 50, kila mwaka tunatoa zaidi ya wahitimu 100,000 utawapeleka wapi kama hukuwapa elimu ya kuwawezesha kujitegemea. Na tumesema vijana aasome katika ilani hii waanzishe kampuni zao zinazoendana na ujuzi wao na sisi tuwape mitaji ili waweze kufanya kazi ya kujiajiri na kuajiri vijana wenzao na hayo wamefanya Korea Kusini na wameweza kwa nini sisi hatuwezi,” ameeleza.
Kuhusu sekta ya afya wlisema ilani ya uchaguzi ya CCM 2020-2030 imeelekeza kuimarisha zaidi huduma za afya “na vile vile tunataka kuwapa bima Watanzania wote wenye uwezo na wasiokuwa nao. Sasa hivi Bunge linatafuta vyanzo vya mapato namna ya kugharamia bima kwa wale ambao hawana uwezo.”
Amesisitiza “Dunia inatuangalia Watanzania wamechagua uchaguzi wameshiriki tunataka tuwashangaze wao na dunia kwamba Watanzania wamekubali uchaguzi na watamchagua Daktari Samia Suluhu Hassan kwa sababu amefanya mambo yanaonekana.”