Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa Ndugu Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na wananchi wa Makunduchi, katika muendelezo wa Kampeni za Uchaguzi kwa CCM, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar tarehe 17 Septemba, 2025.
…………..
NA JOHN BUKUKU – MAKUNDUCHI
Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameende&lea na kampeni zake katika Uwanja wa Kajengwa, Makunduchi wilayani Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar, ambapo ametoa wito wa kulinda na kudumisha amani, mshikamano na tunu muhimu za taifa.
Akizungumza na maelfu ya wananchi na wakazi wa Makunduchi, Dkt. Samia amesisitiza kuwa mshikamano wa Muungano kati ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nguzo muhimu ya maendeleo ya taifa, hivyo kila Mtanzania ana jukumu la kuudumisha.
“Uchaguzi si vita, ni tendo la kidemokrasia. Nawaomba twende tukapige kura kwa amani, kisha turudi nyumbani kwa utulivu. Tuchague viongozi wetu kwa heshima na mshikamano, tukilinda amani ya taifa letu,” alisema Dkt. Samia huku akihimiza wananchi kudumisha utulivu katika kipindi chote cha uchaguzi mkuu.
Aidha, amewahakikishia wananchi kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na vile vya Zanzibar vipo tayari kuhakikisha nchi inabaki salama wakati wote wa uchaguzi, hivyo wananchi wasiwe na hofu.
Dkt. Samia pia aliwaomba wananchi kumpigia kura za ndiyo, akisisitiza kuwa maendeleo ni mchakato unaohitaji mshikamano na mshikikiano wa wananchi na viongozi wao.
Katika hotuba yake, alimpongeza Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Mgombea wa Urais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kwa kuzindua kampeni kwa kishindo kikubwa Septemba 13, 2025, na kuendesha utekelezaji wa Ilani ya CCM 2020–2025 kwa mafanikio makubwa katika sekta za afya, elimu, masoko, makazi na mahakama.
Vilevile, Dkt. Samia aliwataka wagombea wa CCM ngazi za ubunge, uwakilishi na udiwani kuendelea na kampeni zenye kuhamasisha amani, umoja na mshikamano huku wakieleza wananchi utekelezaji wa ahadi za chama na kuomba ridhaa kwa mtaa kwa mtaa na nyumba kwa nyumba.
“Tunapozungumzia mafanikio ya utekelezaji wa Ilani ya CCM, ndiyo maana tuna ujasiri wa kuomba tena ridhaa ya kuongoza nchi kwa miaka mingine mitano. Tuliahidi, tumetekeleza na sasa tunaahidi makubwa zaidi kwa maslahi ya taifa letu,” alisisitiza Dkt. Samia.
Kwa upande wake, Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia CCM, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, alisisitiza kuwa sera ya kwanza ya chama hicho ni kuhimiza amani, mshikamano na maridhiano kwa Watanzania, akibainisha kuwa CCM ndiyo chama kinacholinda tunu kuu za taifa kwa vitendo.
Aidha, aliwaomba wananchi kujitokeza kwa wingi katika mikutano ya kampeni na kushiriki kwa amani katika kupiga kura Oktoba 29, ili chama kiunde serikali imara kuanzia ngazi ya mitaa hadi taifa, kwa lengo la kuendeleza mshikamano na maendeleo ya Watanzania wote.