Na. Sophia Kingimali,Dar es salaam
Mgombea ubunge jimbo la Temeke kupita chama cha wakulima(AAFP)Yusuph Rai ameweka wazi vipaumbele vyake pindi atakapo pewa ridhaa kuongoza jimbo hilo kwa kuhakikisha anakuwa mbunge wa wanachi na sio mbunge wa chama.
Akizungumza leo Septemba 15,2025 wakati akizindua kampeni zake Temeke Jijini Dar es salaam amesema amefikia uamuzi wa kugombea nafasi hiyo baada ya kuona viongozi wote waliotangulia katika jimbo hilo hawajaweza kutatua kero za wananchi.
“Jimbo hili katika miaka yote tumekosa viongozi wanaokwenda kututatulia kero zetu wanaochaguliwa wanafanyakazi kwa ajili ya maslahi ya vyama vyao na maslahi yao binafsi niwaombe wanatemeke sasa chagueni mtu na sio chama kwani ni lazima tupate mabadiliko ya kweli”,Amesema.
Aidha Rai ameongeza kuwa atahakikisha anafanya mabadiliko katika miundombinu mbalimbali ambayo ni changamoto kwenye jimbo hilo ikiwemo miundombinu ya Elimu,Afya,barbara,takataka na miundombinu ya maji safi na salama.
“Mkinichagua nitakwenda kuiambia Serikali kuboresha miundombinu ya elimu kwa kujenga majengo ya ghorofa katika jimbo hili kwani watoto ni wengi na bado wilaya imekuwa nyuma kwenye ufaulu hii tutahakikisha tunapata walimu bora lakini Tozo ya takataka ambayo ni kero tutaifuta badala yake tutazungumza na wawekezaji waliopo katika jimbo hili ili waweze kulibeba jukumu hilo”,Amesema Rai.
Sambamba na hayo amewaahidi wananchi hao atahakikisha soko la Temeke linapanda hadhi na kuwa soko la kimataifa lakini pia kituo kikubwa cha daladala kinajengwa ili kuunganisha barabara na kutoa fursa kwa wafanyabiashara kufanya shughuli zao kwa amani pasipo kusumbuliwa.
Akizungumza changamoto ya maji iliyopo katika jimbo hilo amesema atakwenda kuiambia serikali iweze kuchimba visima vikubwa vya maji katika kila mtu ili wananchi wapate huduma hiyo na kuacha kunywa maji ambayo sio salama kwa afya zao.
“Mabadiliko ni mpango wa Mungu hivyo mabadiliko ni lazima hivyo niwasihi ndugu zangu mkachague kiongozi ambae atasimama na maneno yetu na kero zetu sio maneno yake”,Amesema.
Kwa upande wake mgombea udiwani kata ya Temeke Salumu Tindwa(Kibuda)amesema matatizo ya tandika anayajua hivyo pindi atakapopewa ridhaa na wananchi wa kata hiyo atakwenda kuyashudhilikia ambapo ametaja tatizo kubwa likiwa mikopo ambayo wananchi wamekuwa wakichukua kutoka kwenye taasisi mbalimbali za fedha.
“Nikipata ridhaa hapa nitakwenda kuzungumza na hawa watoa mikopo kupunguza kiwango cha riba wanachotoza lakini namna wanavyodai pindi mtu anapopaswa kutoa rejesho kwa siku husika imekuwa kero nitahakikisha ninakaa nao na kuongea nao”,Amesema.
Aidha ameongeza kuwa atakwenda kuimarisha ulinzi na usalama katika kata hiyo kwa kuwa na ulinzi shirikishi usiku na mchana ambao watakuwa na sare zitakazowatambulisha.
Akizungumza awali kabla ya kumkaribisha mgombea huyo katibu wa itikadi na uenezi Rashid Maokola amesema chama hicho kimempima na kumpika mgombea wake hivyo atakwenda kuleta fikra mpya kwenye maendeleo ya Taifa hivyo wananchi wanapaswa kumuamini na kumpa kura za kutosha ili akafanye mabadiliko ya kweli katika jimbo na Taifa kwa ujumla.