Serikali imewataka mafundi mchundo wa majokofu na viyoyozi kuendelea kutumia njia salama za kuhudumia vifaa hivyo pasipo kuathiri mazingira na sanjari na kuzingatia ukomo wa matumizi wa kemikali zinazodhibitiwa.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Deogratius Paul wakati akifungua mafunzo kwa mafundi viyoyozi na majokofu wa Jiji la Dodoma kuhusu matakwa ya Itifaki ya Montreal kama sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni, leo Septemba 16, 2025.
Tanzania ni nchi mwanachama wa Itifaki ya Montreal ambao unazitaka nchi hizo kutoa mafunzo kwa mafundi viyoyozi na majokofu kuhusu namna bora ya kuhudumia vifaa hivyo pasipo kuachia angani kemikali zinazoweza kusababisha uharibifu wa tabaka la ozoni au kuchangia ongezeko la joto duniani.
Akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo, Dkt. Paul alisema kemikali zinazoharibu tabaka la ozoni ni zile zinazotumika katika majokofu na viyoyozi mbalimbali, vifaa vya kuzimia moto, usafishaji chuma, utengenezaji magodoro, ufukizaji wa udongo katika vitalu vya tumbaku na kilimo cha maua, hifadhi ya nafaka katika maghala na kadhalika.
Dkt. Paul alieleza kuwa kemikali hizo huingizwa nchini kupitia mipaka mbalimbali na zinaweza kuharibu tabaka hilo au kuchangia ongezeko la joto duniani hivyo kusababisha mabadiliko ya tabianchi endapo zikiachiwa angani.
“Tutambue kuwa Tabaka la Ozoni kazi yake kubwa ni kuchuja sehemu kubwa ya mionzi ya jua isifike kwenye uso wa dunia, linapoharibiwa huruhusu mionzi ya jua kufika kwenye uso wa dunia na kusababisha kuongezeka kwa magonjwa mbalimbali yakiwemo saratani ya ngozi, mtoto wa jicho, upungufu wa kinga dhidi ya maradhi na kujikunja kwa ngozi kuathirika kwa ukuaji wa mimea,” alisema.
Aidha, Dkt. Paul ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia Sehemu ya Hifadhi ya Bioanuai aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kuwa mabalozi wa kueneza elimu ya Ozoni kwa wengine ili kuongeza juhudi za kuhifadhi Tabaka la Ozoni na hivyo kuokoa maisha duniani.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi (Sehemu ya Udhibiti wa Uchafuzi wa Mazingira) Idara ya Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Bw. Thomas Chali alisema madhumuni ya itifaki hiyo ni kulinda afya ya binadamu na mazingira dhidi ya madhara yanayotokana na kumong’onyoka kwa tabaka la ozoni yanayotokana na uachiaji angani kemikali zilizothibitishwa kuwa na kiwango kikubwa cha kuharibu tabaka hilo.
Aidha, Bw. Chali alifafanua kuwa kemikali zinazodhibitiwa hutumika katika sekta mbalimbali kama vile majokofu na viyoyozi, kilimo, shughuli za anga, viwanda vya madawa, viwanda vya magodoro na sekta ya uzimaji moto.
Alibainisha kuwa nchini Tanzania, zaidi ya asilimia 90 ya matumizi ya kemikali hizi ni katika sekta ya majokofu na viyoyozi ambapo hutumika kama vipozeo (refrigerants) katika majokofu na viyoyozi.
Mafunzo hayo yamehusisha washiriki 40 wakiwemo mafundi mchundo wa viyoyozi na majokofu kutoka kwenye kampuni binafsi, Watoa mada kutoka:Ofisi ya Makamu wa Rais, Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA)-Chang’ombe na Wakala wa Elimu ya Mafunzo ya Uvuvi (FETA)–Bagamoyo.
Itakumbukwa kuwa kauli mbiu ya Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni mwaka 2025 ni “Miaka 40 ya Mkataba wa Vienna: Mchango wa Sayansi kwenye Jitihada za kimataifa za katika Hifadhi ya Tabaka la Ozoni”.
Kauli mbiu hii imechaguliwa kutokana na Mkataba wa Vienna unaohusu hifadhi ya tabaka la ozoni, kutimiza miaka 40 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1985.