Na Mwandishi Wetu-Kibiti
Mgombea Ubunge wa Jimbo la Rufiji kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Mohamed Mchengerwa amewaahidi wananchi wa Jimbo la Kibiti kuwa, atashirikiana Mgombea Ubunge Jimbo la Kibiti kupitia CCM Bi. Amina Mkumba kuleta maendeleo katika jimbo la Kibiti iwapo wananchi hao watamchagua mgombea huyo wa CCM.
Mchengerwa ametoa ahadi hiyo kwa wananchi wa Kibiti, alipopewa fursa ya kuzungumza na wananchi kwenye wa Uzinduzi wa Kampeni za Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilayani Kibiti.
“Ninawathibitishia wananchi wa Kibiti kuwa sitomtupa Amina, ni msomi na na mwenye uwezo hivyo nitashirikiana nae bega kwa bega kuwaletea maendeleo hapa kibiti, nawasihi mchagueni kwa maendeleo ya Kibiti,” Mchengerwa amesisitiza.
Mchengerwa amefafanua kuwa, ameamua kushirikiana na Amina Mkumba kuleta maendeleo kwani hali za wananchi wa Kibiti bado ni duni kama ilivyo kwa wananchi wa Rufiji na ameongeza kuwa, CCM pekee ndio inaweza kuwaletea maendeleo wananchi wa Kibiti hivyo wasisite kumchagua Amina Mkumba na wagombea Udiwani kupitia CCM.
Aidha, Mchengerwa amewataka wananchi wa Kibiti kumchagua Mgombea Urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kura nyingi za kishindo kwa ajili ya maendeleo endelevu, amani na utulivu wa taifa letu.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu UWT Bi. Susan Kunambi ambaye alikuwa Mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo wa Kampeni za CCM Kibiti, amesema uzinduzi huo ni sehemu ya mkakati wa CCM kujinadi kwa wananchi na kuwaomba kura za ushindi wa kishindo katika ngazi ya Urais, Ubunge na Udiwani ili CCM ipate fursa ya kutekeleza Ilani itakayowaletea maendeleo wananchi.