Na Hafidh Kido
KATIKA Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu 2025, wagombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hadi sasa ni 16 baada ya mgombea wa Chama cha ACT-Wazalendo kuenguliwa ambapo kwa sasa vyama vilivyopo kwenye kampeni ni; CCM, NCCR-Mageuzi, CUF, CHAUMMA,TADEA, TLP, MAKINI, NLD, SAU, DP, UPDP, CCK, AAFP, UMD, UDP na NRA.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) mgombea wake ni Dk. Samia Suluhu Hassan na mgombea mwenza ni Dk. Emmanuel Nchimbi, Chama Cha Wananchi (CUF) kimemsimamisha Gombo Samandito Gombo akiwa na mgombea mwenza Husna Mohamed Abdalla. NCCR-Mageuzi kitawakilishwa na Haji Ambar Khamis pamoja na Dkt. Eveline Wilbard Munisi, huku chama cha CHAUMMA kikiwasimamisha Salum Mwalimu na Devotha Mathew Minja. Katika chama cha UDP, mgombea ni Saum Hussein Rashid, mgombea mwenza ni Juma Khamisi Faki. Chama cha TLP amethibitishwa Yustas Mbatina Rwamugira na Amana Suleiman Mzee.
Chama cha DP amepitishwa Abdul Juma Mluya akiwa na Sadoun Abrahman Khatib, wakati chama cha TADEA kimemsimamisha Georges Gabriel Bussungu kuwania urais na Ali Makame Issa kama mgombea mwenza.
Chama cha UMD, Tume imemthibitisha Mwajuma Noty Mirambo akiwa na mgombea mwenza Mashavu Alawi Haji. UPDP amepitishwa Twalib Ibrahim Kadege na Abdalla Mohamed Khamis. NRA ameteuliwa Hassan Kisabya Almas kuwania urais na Hamis Ali Hassan mgombea mwenza, huku chama cha MAKINI kikiwa na mgombea urais Coaster Jimmy Kibonde na mgombea mwenza Azza Haji Suleiman.
Aidha, Chama cha NLD kitawania urais kupitia Doyo Hassan Doyo pamoja na Chausiku Khatib Mohamed kama mgombea mwenza, wakati SAU kimemsimamisha Majalio Paul Kyara kupeperusha bendera ya chama hicho na Satia Mussa Bebwa. CCK kimempitisha David Daud Mwaijojele na mgombea mwenza Masoud Ali Abdala, huku chama cha AAFP kikiwa na Kunje Ngombare Mwiru kama mgombea urais pamoja na Chumu Abdallah Juma, mgombea mwenza.
Katika mazingira ya kisiasa ya Tanzania, uchaguzi Mkuu wa 2025 unaleta changamoto nyingi lakini pia fursa kwa Dk. Samia Suluhu Hassan, kushinda tena.
Hata hivyo, mbali ya mgombea wa CCM, Dk. Samia kuwa na turufu ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini chama chake kimejiandaa vema kwa ushindi, hawajabweteka.
Mafanikio makubwa aliyoyaonyesha katika kipindi kifupi cha miaka mnne aliyokabidhiwa ofisi yanamfanya kuwa mgombea anayekubalika na wananchi wengi hasa walio vijijini.
Ambao, kwa kiasi kikubwa waliteswa na kukosena huduma muhimu za maji safi na salama, huduma za afya hasa mama na mtoto Pamoja na miundombinu ya barabara kwa wafanyabiashara na mbolea za ruzuku kwa wakulima.
Katika mikoa ambayo reli ya kisasa (SGR) imepita na inatarajiwa kupita ikiwemo Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Dodoma, Singida, Tabora na Kigoma wananchi wanaonyesha furaha yao na maneno yao daima yanafanana kuwa hawana cha kumlipa zaidi ya kumpigia kura ili amalizie aliyoyaanza.
Hata sasa wakati kampeni zinaendelea, ahadi alizozitoa akiwa kwenye ziara za kikazi mikoani ikiwemo Umeme, miradi ya maji na barabara za vijijini na mijini kazi inaendelea kufanyika wakandarasi wakiwa kazini au zabuni zinatangazwa ili waanze kazi, si mambo ya paukwa pakawa au hadithi za abunuwasi, bali ni mambo yanayoonekana kwa macho na kushikika kwa mikono.
Vilevile, kitendo cha asilimia kubwa ya maeneo ya vijijini kupata huduma bora za afya na elimu, vitu ambavyo kabla ya kukalia kiti cha urais ilikuwa changamoto ambayo utawala wake umeanza kushughulikia.
Kitu cha kipekee ambacho huwezi kukiona kama huna jicho la kiuchambuzi ni uimara wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho kina mizizi na mtandao mkubwa wa wafuasi, hasa vijijini.
Hii inampa nafasi Dk. Samia kusimama popote kunadi sera za chama hicho. Pia, chama kina rasilimali watu, viongozi wakuu wastaafu wa chama na serikali, wamekabidhiwa jukumu la kuratibu Kanda 11 za kichama ndani ya uchaguzi wa mwaka huu.
Katika maeneo yote aliyopita kuomba kura, Dk. Samia ameweka mkazo mkubwa katika afya, elimu, uanzishwaji viwanda vidogo (SMEs), na kuimarisha huduma za jamii kwa makundi ya watu walio hatarini (wazee, wajawazito, watu wenye ulemavu).
Ahadi yake katika safari ya uchaguzi mkuu Oktoba 29, 2025 ni kuhakikisha huduma ya afya ya msingi inapatikana kwa wote, na kuanzisha mfumo wa bima ya afya kwa jamii. Ahadi kama hizi huzidisha matumaini miongoni mwa wapiga kura ambao hukumbwa na adha ya kukosa huduma muhimu za afya kwa sababu ya hali duni za maisha lakini pia umbali wa kupatikana huduma hiyo.