NA JOHN BUKUKU- DAR ES SALAAM
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea na ratiba yake ya kampeni kwa kuwasili visiwani Zanzibar jana jioni mara baada ya kukamilisha kampeni mkoani Kigoma.
Akiwa mjini Kigoma jana, Dkt. Samia alihitimisha kampeni zake kwa kuwataka wananchi wa mkoa huo kuendelea kushirikiana na serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo mikubwa inayotekelezwa, ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR, maboresho ya bandari na barabara za kimkakati ambazo zitaufanya mkoa huo kuwa kitovu cha biashara na uchumi.
“Tumefanya mengi Kigoma, na tunaendelea kufanya zaidi. Miradi ya reli, barabara na umeme wa bwawa la Malagarasi itaufanya mkoa huu uwe lango kuu la biashara na maendeleo. Nina imani mtaniamini tena ili tuendelee na safari ya kuijenga Tanzania,” alisema Dkt. Samia katika hotuba yake ya kufunga kampeni Kigoma.
Baada ya kukamilisha ratiba hiyo, Dkt. Samia aliwasili Zanzibar ambapo alipokelewa na viongozi wa CCM pamoja na wananchi waliojitokeza kumpokea katika Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume.
Mikutano ya kampeni za CCM kisiwani Zanzibar zinatarajiwa kuanza rasmi Septemba 17, ambapo Dkt. Samia ataendelea kueleza ilani ya chama chake na kuomba ridhaa ya wananchi wa visiwani humo kuendeleza kasi ya maendeleo ya taifa.