NA JOHN BUKUKU- KIGOMA
MGOMBEA Urais wa CCM Dkt Samia Suluhu amesema kutokana na kasi ya maendeleo anayoiona, mkoa wa Kigoma utakuwa kitovu cha Uchumi na Biashara kutokana na kwamba reli haitaishia hapo, bali itapita kuelekea nchi za Burundi mpaka DRC Kongo.
Dkt Samia aliyasema hayo leo wakati akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya Katosho Bandari Kavu mjini Kigoma, Septemba 14, 2025, katika muendelezo wa kampeni zake kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
Alisema kwamba siku za nyuma walikuwa wamezoea kusema Kigoma ni mwisho wa reli, lakini kutokana na kasi kubwa ya maendeleo anayoiona sasa, mkoa huo utakwenda kuwa kitovu cha uchumi na biashara.
“Siku za nyuma tulikuwa tumezoea kusema Kigoma ni mwisho wa reli, lakini kwa kasi ya maendeleo ninayoiona sasa, mkoa huo huo utakuwa kitovu cha uchumi na biashara. Maana hata reli yenyewe haitaishia Kigoma, itapita kwenda Burundi na inasonga mbele mpaka DRC. Hivyo Kigoma sio tena mwisho wa reli,” alisema.
Ameeleza kuwa kwa sasa Serikali inafanya maboresho ya viwanja vya ndege 14 Tanzania, ambapo sita vimekamilika na vinane vinaendelea kukamilishwa. Alibainisha kuwa Serikali imejidhatiti kuunganisha mkoa huo kwa njia zote za anga, maji, reli na barabara.
Aidha alisema tayari maboresho ya uwanja wa ndege yanaendelea, na njia imeanza kutumika huku jengo likiendelea kujengwa. Mradi huo ni mpango mpana wa kitaifa wa kuifungua anga la Tanzania na kuimarisha Shirika la Ndege la Air Tanzania, ambapo ndege zake zinatua mkoani humo na wanatarajia kuanzisha safari za ndege kwenda Lagos, Nigeria.
Akizungumzia reli ya Kigoma, Dkt Samia alisema kwamba ni sehemu muhimu ya reli ya SGR, kwani kuna vipande viwili: kipande cha sita Tabora–Kigoma na kipande cha saba Uvinza–Msogati. Baada ya kufika Kigoma reli hiyo itakwenda Burundi na hatimaye mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
“Mmeshaona tumekamilisha sehemu ya kwanza na ya pili ya Dar hadi Dodoma, na sehemu zote zilizobaki ya tatu na ya nne na ya tano, ambayo ni Mwanza–Isaka, itakamilika mwaka huu. Na ya sita ambayo ni Tabora–Kigoma na ya saba Uvinza–Msogati kazi inaendelea,” alieleza Dkt Samia.
Alisema sambamba na SGR, wanaiboresha reli ya zamani ya MGR ambapo tayari wamenunua vichwa vya treni vitatu vipya, mabehewa mapya ya abiria 22 na ya mizigo 44. Aidha, mabehewa 350 ya mizigo na 33 ya abiria yanafanyiwa ukarabati na mengi yameshakamilika.
Kazi hiyo imefanyika kwa kushirikiana na wabia wa maendeleo waliokarabati mabehewa 90 pamoja na mengine 8 yanayotunza ubaridi kwa ajili ya kusafirisha mazao ya matunda na mbogamboga.
“Vilevile tumefanya maboresho ya kanuni kuhusu waendeshaji wa huduma ndani ya reli, na sasa zinaruhusu waendeshaji binafsi kufanya biashara kwenye miundombinu ya reli iliyotandikwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo mambo ya operesheni ya uendeshaji watafanya Serikali na watu binafsi. Wale ambao tutawaona wanaweza kuendana na sisi tutawaruhusu wawekeze kuleta ufanisi wa usafirishaji mizigo na usafirishaji abiria ili uchumi wetu ufunguke,” alisema.
Kwa upande wa usafiri majini, alisema wametekeleza miradi mikubwa kwenye maziwa makuu ikiwemo ujenzi na ukarabati wa bandari na meli za abiria na mizigo. Kwa upande wa Ziwa Tanganyika hususani Mkoa wa Kigoma, Serikali imeendelea na ujenzi na ukarabati wa Bandari ya Kibiriti, Kabwe na Kigoma.
Aidha, Serikali pia imeendelea na ujenzi na ukarabati wa Bandari ya Karema iliyopo mkoani Katavi na Bandari ya Kasanga iliyopo mkoani Rukwa.
Katika hatua nyingine, Dkt Samia alimuelezea aliyekuwa Makamu wa Rais, Dkt Philip Mpango, kuwa ni mwadilifu, mchapakazi na mzalendo katika nafasi zote alizowatumikia Watanzania.
“Dkt Mpango amenisaidia sana kipindi cha miaka minne iliyopita na kuwa sehemu ya mafanikio yaliyopatikana. Na niseme kwamba bado ataendelea kutusaidia kama sehemu ya kutekeleza yanayokuja mbele yetu,” alisema.