NA DENIS MLOWE, IRINGA
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira leo amezindua rasmi kampeni za uchaguzi katika Jimbo la Kalenga, mkoani Iringa na kuwataka wananchi kuendelea kuichagua CCM kwa lengo la kuwaletea maendelelo na kudumisha amani iliyoko nchini.
Uzinduzi huo umefanyika katika uwanja wa Kidamali na kuhudhuliwa na Viongozi mbalimbali wa CCM mkoa wa Iringa akiwemo MCC Salim Abri na maelfu ya wananchi wa jimbo la Kalenga.
Katika hotuba yake kwa wananchi wa Kalenga, Makamu Mwenyekiti Wasira alisema kuwa CCM ni mwendelezo wa mapambano ya uhuru, uchumi na ustawi wa jamii na kusisitiza kuwa chama hicho kina sababu ya kuomba kura kutokana na utekelezaji mzuri wa Ilani ya uchaguzi katika miaka mitano iliyopita, tofauti na vyama vingine ambavyo havina historia ya kutekeleza.
Wasira ametaja baadhi ya vipaumbele vya Ilani ya CCM ya mwaka 2025–2030, ikiwa ni pamoja na kujenga shule tano za msingi na sekondari, kuanzisha vituo vya afya, kuongeza huduma za kijamii, na kuboresha sekta ya kilimo kwa kutoa ruzuku kwa wakulima, kusambaza mbolea kwa wakati, na kuanzisha vituo vya zana za kilimo na ufugaji.
Aidha, alimkabidhi Kiswaga Ilani ya CCM ya Kitaifa pamoja na ya Mkoa wa Iringa ili aweze kufahamu kikamilifu mpango wa maendeleo ya Jimbo la Kalenga. Ameeleza kuwa Kiswaga ni kiongozi mzoefu, anayeifahamu Kalenga vizuri na anastahili kupewa nafasi ya kuendelea kuwatumikia wananchi.
Jackson Kiswaga ambaye hivi karibuni alitangazwa rasmi kuwa mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM alipongezwa na Makamu kutokana na kuchaguliwa tena kutokana na kasumba iliyozoeleka kwamba jimbo la Kalenga huwa mbunge hachaguliwi mara mbili.
Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Taifa, Salim Abri Asas, alitumia fursa ya mkutano huo kumwomba Makamu Mwenyekiti Stephen Wasira kufikisha salamu kwa Mwenyekiti wa Chama hicho akisema kuwa wananchi wa Kalenga ni waaminifu, na wanapotoa ahadi huwa hawabadiliki.
Alisisitiza kuwa kura zote zitakwenda kwa CCM kwa nafasi ya Urais, Ubunge na Udiwani, wakiamini katika dira ya maendeleo ya chama hicho.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daud Yassin, amesema kuwa serikali ya awamu ya sita imetekeleza miradi mikubwa ya maendeleo mkoani humo, hususan kwenye sekta za maji, nishati, barabara na afya akieleza kuwa utekelezaji huo unadhihirisha dhamira ya kweli ya CCM katika kuwaletea wananchi maendeleo ya maana.
Kwa upande wake mgombea ubungejimbo la Kalenga, Jackson Kiswaga aliwashukuru viongozi wa CCM kwa kumuamini na kumteua kugombea tena.
Alisema kuwa tarehe 29 Oktoba, wananchi wa Kalenga watachagua kwa kishindo Chama Cha Mapinduzi, akieleza kuwa miradi mingi imetekelezwa na mingine inaendelea, ikiwa ni ushahidi wa utekelezaji madhubuti wa Ilani ya CCM.
Kiswaga aliwataka wananchi kusimama imara na kuhakikisha wanachagua viongozi wa CCM kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge hadi urais, kwa kuwa chama hicho kina dira, sera na utekelezaji unaogusa maisha ya wananchi wa kawaida.