Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Hasani Kabeke (katikati), akisoma tamko la kuombea uchaguzi, amani ya nchi na Marais, Dk.Samia Suluhu Hassan na Dr. Hussen Mwinyi, mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani), leo ofisini kwake.Kushoto ni Katibu wa BAKWATA, Ustadhi Ramadhan Chanila, kulia ni Sheikh wa Wilaya ya Ilemela, Abdulwarith Jumaa.
Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Hasani Kabeke (katikati), akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) leo, mara baada yab kusoma tamko la kuombea uchaguzi mkuu 2025, amani ya nchi na Marais, Dk.Samia Suluhu Hassan na Dr. Hussen Mwinyi. (Picha na Baltazar Mashaka )
……..
NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Alhaji Hasani Kabeke, leo ametoa tamko maalum mbele ya waandishi wa habari jijini hapa, akiwahimiza Waislamu wa mkoa huo na Watanzania kwa ujumla kutekeleza mambo matatu ya msingi kwa mustakabali wa dini, taifa, na amani ya nchi yetu.
Tamko hilo linatokana na agizo la Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Abubakar Zuber bin Ally Mbwana, alilolitoa wakati wa Maulidi ya Kitaifa yaliyofanyika Korogwe, mkoani Tanga, Septemba 4, 2025, kutokana na uzalendo, mwenye mapenzi na uchungu kwa nchi yake.
Katika agizo hilo, Mufti wa Tanzania, Abubakar Zuber alihimiza Waislamu kote nchini kufunga Swaumu maalum na kufanya dua kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa 2025, amani na utulivu wa taifa, viongozi wakuu wa nchi, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Zanzibar, Dr. Hussein Ali Mwinyi
“Nimeiwata hapa kwa unyenyekevu mtusaidie kupaza sauti na kuwafikishia Watanzania hususani wa Mwanza, Waislamu na wasio Waislamu agizo la Mufti kuhusu ibada ya Swaumu na dua ya kuombea uchaguzi mkuu, Rais Dk.Samia na Dr. Mwinyi,” alisema Sheikh Kabeke.
Alisema kuwa BAKWATA Mkoa wa Mwanza imepokea agizo hilo na linaungwa mkono kikamilifu kwa kuwa nchi ipo katika mchakato wa kuelekea uchaguzi mkuu, hivyo ni wajibu wa kila Mwislamu na Mtanzania kumuomba Mwenyezi Mungu ailinde nchi, awaongoze viongozi waliopo madarakani na kuwezesha uchaguzi wa amani na haki.
“Ni wajibu wetu wa kidini na kijamii kuwaombea dua viongozi wetu ili waendelee kuongozwa kwa hekima na busara. Agizo hili tumelipokea kwa mujibu wa Katiba ya BAKWATA, nami nikiwa sheikh wa mkoa na msimamizi wa nidhamu ya Waislamu katika mkoa, nalitekeleza ipasavyo,” alisema Sheikh Kabeke.
Aidha, Sheikh huyo akinukuu maneno ya Mufti Abubakar Zuber, aliwataka Watanzania kutotumia visingizio wala kujidhulumu haki yao ya kikatiba,akiwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki kampeni, kuwasikiliza wagombea wa vyama vyote vinavyoshiriki uchaguzi, na hatimaye kujitokeza kupiga kura kwa amani ili kuchagua viongozi bora wa kuwaletea maendeleo.
“Pamoja na mambo mengine, Mufti aliwataka Watanzania wasijidhulumu wenyewe, katika mchakato wa uchaguzi waende kwenye mikutano ya kampeni bila kubagua, wakasikilize na kuwapima wagombea wa vyama vyote, kwa sababu ni haki yao ya kikatiba na kdemokrasia,baada ya kuwasikiliza siku ikifika wakapige kura,” alisema.
Sheikh Kabeke aliongeza; “Asitokee Mtanzania akasema sipigi kura hapana, tuhakikishe kila mwananchi mwenye sifa anatimiza wajibu wake, kupiga kura ni haki yako na kwa sura hiyo Mufti Abubakar Mbwana aliwaeleza masheikh kuanzia mkoa, wilaya na kata pamoja na Watanzania wenye mapenzi mema kuiombea nchi.”
Hivyo, tamko hilo linaakisi mshikamano wa kitaifa uliopo, ushiriki wa raia katika mchakato wa kidemokrasia, nafasi ya maombi katika kulinda amani na kuimarisha uongozi bora.
Aidha, Sheikh Kabeke aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa kutambua heshm na thamani ya Mtume Muhammad S.A.W, imekuwa ya pekee duniani kwa kutenga siku maalum ya kuadhimisha kuzaliwa kwake, ni fursa ya kujifunza mafundisho na maadili ya Kiislamu.
“ Kwa niaba ya Waislamu wa Mkoa wa Mwanza,alitangaza Maulidi ya mkoa yatakayofanyika Septemba 27, mwaka huu, katika Msikiti wa Allah Karim Pasiansi, wilayani Ilemela, kabla ibada ya Swaum itaanza Septemba 22,2025,”alisema.
Katika hatua nyingine alitangaza kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo wa Mufti (MDF), mkoani Mwanza,ukilenga kusaidia miradi ya elimu, afya, uchumi wa Waislamu,kuwezesha misikiti, taasisi na vikundi vya maendeleo, kupanga na kutoa msaada ya kijamii na dharura.
“Wito wangu kwa Waislamu na wadau wote wa maendeleo, tushirikiane kwa hali na mali kuimarisha mfuko huu kwa manufaa ya dini, jamii na taifa pia, ntume fursa hii kuwaomba wadau wa amani,vyombo vya habari,viongozi wa dini na wanaharakati wa kijamii, kueneza ujumbe huu,”alisema Sheikh Kabeke .