Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
Septemba 12, 2025
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Pwani imerejesha zaidi ya milioni 1.3 kwa wananchi wa Kitongoji cha Nyakahamba, kata ya Kerege, wilayani Bagamoyo, waliotozwa kinyume cha utaratibu na Mwenyekiti wa Kitongoji kwa ajili ya kulipia huduma ya maji, licha ya kuwa mkandarasi wa mradi tayari alikuwa amelipwa.
Akitoa taarifa kuhusu ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo kwa kipindi cha Aprili hadi Juni 2025, Domina Mukama, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Pwani, amesema urejeshwaji huo wa fedha ni sehemu ya mafanikio ya jitihada za taasisi hiyo katika kuhakikisha fedha za umma zinatumika ipasavyo.
Kwa mujibu wa Mukama, ufuatiliaji huo ulifanyika katika mradi wa upanuzi wa vituo vya kuchotea maji katika Kitongoji cha Nyakahamba, wenye thamani ya shilingi milioni 60.
Amebainisha, uchunguzi wa TAKUKURU ulibaini kuwa wananchi hawakustahili kulipia huduma ya maji, kwani mkandarasi alikuwa tayari amelipwa gharama zote za kipindi cha majaribio, kabla ya mradi kukabidhiwa kwa RUWASA (Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini), kata ya Mapinga, kwa ajili ya uendeshaji rasmi.
Ameeleza , hadi kufikia kipindi hicho TAKUKURU imefuatilia jumla ya sh. bilioni 32.7 zilizotumika katika miradi 40 ya maendeleo kutoka sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, na barabara.