NA JOHN BUKUKU- ILOLANGULU- TANORA
……….
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema serikali itaendelea kuajiri watumishi wa afya na kada nyingine ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa watumishi katika sekta hizo muhimu.
Akihutubia mkutano wa kampeni katika Kata ya Ilolangulu, Wilaya ya Uyui mkoani Tabora, Dkt. Samia alisema tayari walimu 412 wameajiriwa kwa ajili ya shule za wilaya hiyo na watumishi wa afya 161 pia wamepelekwa katika vituo mbalimbali vya kutolea huduma.
“Kama nilivyowaambia, ndani ya siku mia za mwanzo mkinipa ridhaa ya kuongoza nchi hii tena, tutaajiri watumishi wapatao elfu tano kwenye sekta ya afya na watumishi elfu saba katika sekta ya elimu. Lengo letu ni kupunguza uhaba uliopo na kuhakikisha huduma muhimu zinapatikana kwa wananchi,” alisema.
Alibainisha kuwa zaidi ya shilingi bilioni 8 zimetumika kuboresha sekta ya afya katika Wilaya ya Uyui, ikiwemo kuimarisha hospitali ya wilaya, kujenga vituo vipya vitano vya afya na zahanati 17, na kufanya jumla ya zahanati zilizopo sasa kufikia 57. Aidha, magari matatu ya wagonjwa yameletwa na yanafanya kazi ya kuwahudumia wananchi.
Kwa upande wa elimu, Dkt. Samia alisema shule za sekondari zimeongezwa kutoka 27 hadi 34 na shule za msingi zimeongezeka kutoka 154 hadi 182, huku idadi ya wanafunzi ikipanda kutoka 12,000 hadi zaidi ya 17,000. Pia, serikali imeendelea kusimamia sera ya elimu bila malipo kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha sita pamoja na kujenga madarasa ya chekechea ili kuweka msingi mzuri wa elimu ya awali.
Katika hotuba hiyo, Dkt. Samia pia aliahidi kushughulikia madai ya wakulima wa tumbaku wanaodai malipo yao kwa muda mrefu. Alisema serikali ipo kwenye mazungumzo na kampuni zinazodaiwa na wakulima na malipo yatafuatiliwa kwa karibu kupitia Wizara ya Kilimo.
“Wakulima wa tumbaku wameongeza uzalishaji kutokana na mbolea na pembejeo tunazotoa. Tanzania sasa inauza tumbaku kwa kiwango kikubwa, na fedha wanazodai wakulima zitalipwa kupitia usimamizi wa Waziri wa Kilimo,” alisema.
Mbali na hayo, Dkt. Samia alieleza kuwa serikali imeendelea kuwekeza kwenye sekta ya maji kwa kutekeleza miradi 15 ya kuongeza upatikanaji wa maji. Pia, kupitia mradi wa Ziwa Victoria, tanki kubwa la lita milioni moja litajengwa katika eneo la Ilolangulu ili kuhudumia wananchi.
Aidha, usanifu na gharama za daraja la Mto Loya zimekamilika na fedha zimetengwa tayari, ambapo ujenzi wa daraja hilo utasaidia wananchi kuvuka kwa urahisi kipindi cha masika.