NA JOHN BUKUKU- KALIUA TABORA
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, amewaahidi wakazi wa Kaliua mkoani Tabora kuwa endapo chama hicho kitapata ridhaa ya kuongoza nchi, kitajenga mabwawa na skimu za umwagiliaji.
Mgombea huyo alisema hayo Septemba 11, 2025 wilayani Kaliua mkoani Tabora, wakati akiomba kura kwa wananchi na kueleza sera za CCM ambazo zitamuongoza katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Ndugu zangu, pamoja na mambo mengine, Ilani hii imetuelekeza mkitupa ridhaa yenu tukiunda serikali twende tukafanye ujenzi wa mabwawa na skimu za Kona Nne, Igombe, Mnange, Libula na Igwisi.
“Huko ni mabwawa na skimu za umwagiliaji maji lakini vilevile kuwezesha mradi wa Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) wa kilimo na mifugo ndani ya wilaya hii. Huu ni mradi maalum kwa vijana. Jenga Kesho Iliyo Bora kwenye mashamba ya kilimo lakini pia ya mifugo. Ndugu zangu, kwa wilaya hii ya Kaliua Ilani imetuelekeza tufanye ujenzi wa chujio la kutibu maji ya Bwawa la Ichemba na bwawa la ujenzi wa mradi wa maji wa vijiji 17,” alisema Dk. Samia.
Dk. Samia alivitaja vijiji hivyo kuwa ni Ibambo, Muongozo, Mwanduti, Kanindo, Kanoge, Ichemba, Uranga, Makingi, Mjelela, Twigu, Nhandwe, Mwamashimba, Utandamke, Veta, Mapigano, Upendano, Imagi, Ikonongo, Kaswa, Makonge na vingine.
Alisema vijiji hivyo vitapatiwa maendeleo na kukamilishiwa miradi ya maji ili viweze kupata maji safi na salama.
“Upande mwingine tumeelezwa kujenga Bwawa la Mzugimlole, hili ni bwawa la maji ili wananchi waweze kupata maji. Miradi mingine ya maji ni ujenzi wa mradi wa maji katika vijiji vya Kaswakanindo, Ugunga na Ligumba, Imaraupina, Nhandwe, Ugasa, Mpandamlowoka pamoja na Msungwa, Ikonongo na Usigala,” alisema Dk. Samia.
Dk. Samia alisema miradi ya maji inaendelea, lakini katika awamu ya pili ya mradi wa maji wa vijiji vya Usinge na Ulindwanoni, wanatarajia kumaliza kabisa changamoto ya maji iliyopo.
“Kwa hiyo tunaendelea na miradi ya maji katika maeneo kadhaa pamoja na uchimbaji wa visima, lakini miaka mitano inayokuja tunataka tumalize kabisa shida ya maji ndani ya Wilaya hii ya Kaliua.
“Ndugu zangu, mambo mengine tuliyoelekezwa ni kuanzisha ranchi, shamba la malisho na uhamilishaji ndani ya wilaya hii, lakini pia ujenzi wa mnada na machinjio ya kisasa kule Kasungu. Tutakwenda kuweka mnada mpya wa kisasa na machinjio ya kisasa.
“Jambo jingine ni ujenzi wa majosho ya mifugo kule Makingi na Mitimitano, ambako nako kutajengwa majosho ya mifugo. Pia tutakamilisha ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Kaliua.
“Kuna majengo hayajakamilika, tunakuja kuyatimiza yote, ikiwemo majengo ya afya ya mama na mtoto. Tutakamilisha yote kwenye Hospitali ya Kaliua,” alisema Dk. Samia.