Na Silivia Amandius.
Bukoba, Kagera.
Vijana mkoani Kagera wametakiwa kutumia kikamilifu fursa mbalimbali za maendeleo zinazotolewa na Serikali, hasa katika sekta za kilimo, ufugaji, na ufundi. Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mkoa wa Kagera, Faris Buruhan, wakati wa tukio la mbio za Mwenge wa Uhuru lililofanyika katika Manispaa ya Bukoba.
Faris amesema kuwa mabadiliko ya kiuchumi na kijamii yanayoshuhudiwa mkoani humo ni matokeo ya jitihada za Serikali katika kuhakikisha vijana wanakuwa sehemu ya maendeleo ya taifa. Ameeleza kuwa vijana wengi wamewezeshwa kupitia miradi ya kijamii na kiuchumi inayolenga kuinua maisha yao.
Amehimiza vijana kutambua mchango wao katika kujenga taifa, hasa kwa kutumia ujuzi na maarifa waliyonayo katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo. Aidha, amesisitiza umuhimu wa ushiriki wa vijana katika shughuli za kijamii na za kujitolea kama njia mojawapo ya kuonesha uzalendo na uwajibikaji kwa jamii
Katika kuhitimisha, Faris amesema vijana wa Kagera wameonyesha nia ya dhati kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maendeleo, huku wakipongeza juhudi mbalimbali za Serikali katika kuwaletea huduma bora na kuwawezesha kiuchumi.