Na Meleka Kulwa -Dodoma
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Ushirika (Coop Bank), Godfrey Ng’urah, amesema ushirikiano kati ya benki hiyo na Shirika la Bima la Taifa (NIC) unalenga kujibu changamoto za muda mrefu za ukosefu wa bima mahsusi kwa sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi nchini.
“Tutaangazia sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi pamoja na mnyororo wa thamani wa kilimo biashara. Tunaingia na bima zitakazojibu ukosefu wa bima katika sekta ya kilimo biashara. Kwa kushirikiana na NIC, tutatoa huduma hizi kwa niaba yao kwa wateja wetu,” amesema Ng’urah leo Jumatano, Septemba 10, 2025 jijini Dodoma wakati wa hafla ya kusaini mkataba wa makubaliano ya kibiashara.
Aidha, Amesema kuwa zaidi ya asilimia 65–70 ya Watanzania wanaishi vijijini na uchumi wao unategemea kilimo, hasa kupitia vyama vya ushirika. Aidha, kuna zaidi ya vyama vya msingi vya kilimo 6,000 vyenye wanachama milioni 8 pamoja na vyama vya fedha (SACCOS) karibu 2,000 vyenye wanachama milioni 2.
Ng’urah amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Kilimo na Ushirika imechukua hatua ya kuwaunganisha wakulima zaidi ya milioni 10 walioko chini ya vyama vya ushirika ili waweze kunufaika na huduma za mikopo na bima ikiwemo Shirika la Bima la Taifa (NIC). Amebainisha kuwa lengo ni kuwawezesha wakulima kulinda uwekezaji wao na kuongeza tija katika kilimo kwa ujumla.
Pamoja na mchango mkubwa wa kilimo kwenye uchumi wa taifa, taarifa zinaonesha kuwa sekta hiyo imekuwa ikipata sehemu ndogo ya mikopo ya kifedha. Kati ya Shilingi trilioni 40 zilizotolewa kwa ajili ya mikopo nchini, ni trilioni 3.8 pekee ndizo zilizoelekezwa kwenye sekta ya kilimo, mifugo, uvuvi na biashara zinazotokana na sekta hizo.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa NIC, Abdi Mkeyenge, amesema kuwa shirika hilo limejipanga kusaidia ukuaji wa uchumi wa taifa kupitia uwekezaji wa ada za bima kwenye benki za biashara nchini.
“Benki hii ikiwa na nguvu basi vyama vyenyewe vitakuwa na nguvu na wamiliki watafaidika, lakini pia tunamwangalia mkulima wa chini ambaye anatakiwa kuinuliwa. Sekta ya kilimo ni muhimu sana kwa ukuaji wa uchumi wa nchi yeyote, hasa sisi ambao tumebarikiwa eneo kubwa la kufanya kilimo,” amesema Mkeyenge.
Amefafanua kuwa NIC inatoa huduma za bima za maisha, mali, ajali na majanga, pamoja na bima za credit life ambazo hulinda dhidi ya upotevu wa fedha, akisisitiza kuwa ushirikiano huo na Coop Bank ni mkakati wa “kubakisha uchumi ndani ya nchi” kupitia uwekezaji wa ndani.
Makubaliano hayo yanalenga kutoa huduma jumuishi za kifedha na bima kwa wakulima kupitia vyama vya ushirika, hatua inayotarajiwa kuongeza upatikanaji wa mitaji kwa shughuli za kilimo, kupunguza athari za majanga, na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika pato la taifa.
Ushirikiano huo unatarajiwa kuongeza wigo wa huduma za kifedha na bima hadi kufikia zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania wanaojihusisha na kilimo vijijini, hatua inayotajwa kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya uchumi wa kilimo nchini.