Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Saipulan Ramsey akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Arusha.
………,.
Happy Lazaro, Arusha.
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza rasmi ziara ya mgombea mwenza wa urais, Dkt. Emmanuel Nchimbi, mkoani Arusha, itakayofanyika Septemba 12, 2025.
Aidha kufuatia ziara hiyo wananchi wamehimizwa kujitokeza kwa wingi kumpokea kiongozi huyo na kuweza kusikiliza sera za chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo ofisini kwake jijini Arusha, Katibu wa Itikadi, Siasa na Uenezi wa CCM mkoa huo, Saipulan Ramsey, amesema maandalizi yote yako tayari na chama kinatarajia mapokezi makubwa kutoka kwa wanachama na wananchi kwa ujumla.
“Tunawaomba wananchi na wafuasi wa
CCM kufika kwa wingi kwani huu ni mkutano wa kihistoria ambapo Dkt. Nchimbi atamwombea kura Rais Samia Suluhu Hassan na mgombea ubunge wa Jimbo la Arusha, Paul Makonda,” amesema Ramsey.
Aidha Ramsey amesema kuwa, ataanzia ziara yake wilayani Longido,kisha ataelekea Arumeru ambapo atafanya mkutano katika barabara ya Bypass. Ziara hiyo itahitimishwa kwa mkutano mkubwa jijini Arusha utakaofanyika katika Uwanja wa Soweto kuanzia majira ya saa saba mchana.
Remsey amesisitiza kuwa CCM imedhamiria kuhakikisha wananchi wanahudhuria kwa wingi bila vikwazo vya usafiri.
“Sasa hivi tunatumia mabasi kuwabeba wafuasi wetu na siyo tena punda. ,tmunawahakikishia usafiri wa uhakika ili kila mmoja afike kwa wakati. Raha ya mwanasiasa ni kuona uwanja umefurika wananchi wenye hamasa,” ameongeza Ramsey .
Aidha Ramsey amesema kuwa mkutano huo utapambwa na magari yenye rangi za mabakamabaka ya mgombea Ubunge wa jimbo la Arusha, Paul Makonda, na kuwatoa hofu wananchi wanaohofia kwamba ni magari ya jeshi la wananchi JWTZ.
“Tunatarajia kusikia mipango ya chama chetu kuendelea kuboresha maisha ya wananchi. Ujio wa Dkt. Nchimbi unatupa matumaini makubwa ya ushindi.”