NA JOHN BUKUKU – NZEGA TABORA
Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amepongeza Mbunge wa Nzega Mjini na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, kwa mchango wake mkubwa katika sekta ya kilimo hususan kwenye miradi ya umwagiliaji.
Dkt. Samia amesema kuwa miradi yote inayotekelezwa nchini imewezekana kutokana na usimamizi thabiti wa fedha za umma na kupunguza mianya ya rushwa, hatua iliyowezesha Tanzania kupiga hatua kubwa za maendeleo.
Amesema serikali ya CCM itaendeleza miradi ya maendeleo endapo watapewa ridhaa ya kuongoza tena nchi kwa kipindi cha miaka mitano ijayo (2025–2030).
Aidha, amewapongeza wachimbaji wadogo wa dhahabu wa Lusu kwa mchango wao mkubwa katika mapato ya serikali, akisema kuwa wachimbaji wadogo huchangia asilimia 40 ya mapato yatokanayo na madini.
Amesema pia serikali itaendelea kuwaendeleza wachimbaji hao kupitia mipango mbalimbali.
Akizungumza na wananchi na wakazi wa Nzega, Dkt. Samia ameahidi ujenzi wa soko jipya kupitia mradi wa TACTIC sambamba na barabara za lami zenye urefu wa kilometa 10 ndani ya mji wa Nzega.
Aidha, amesema kuwa serikali itajenga machinjio manne na majosho sita kwa ajili ya wafugaji wa wilaya hiyo, pamoja na kuendelea kutoa ruzuku za chanjo kwa mifugo.
Katika sekta ya maji, amebainisha kuwa awamu ya pili ya mradi wa maji kutoka Ziwa Viktoria itakapokamilika, wananchi 85,607 watanufaika.
Kuhusu miundombinu ya barabara, Dkt. Samia ameahidi kukamilisha ujenzi wa barabara ya Nzega–Itobo–Kagongwa yenye urefu wa kilometa 65, pamoja na barabara za kiwango cha lami katika maeneo ya Choma–Ziba na Mkinga–Simbo–Puge.
Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, amesema kuwa hatua kubwa zilizochukuliwa katika sekta ya kilimo, ikiwemo ruzuku ya zaidi ya shilingi bilioni 13 kwa wakulima wa tumbaku na uzalishaji wa tani 188,000, ni kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa tangu uhuru.
Amesema Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imejipanga kukabiliana na kesi zinazopinga uzalishaji wa tumbaku, akisisitiza kuwa tumbaku ni maisha ya Watanzania.
Aidha, amesema kuwa kuna mchango mkubwa wa ruzuku kwa wakulima wa pamba katika Mkoa wa Tabora, ikiwemo Wilaya ya Igunga, ambapo uzalishaji umeongezeka kutoka tani 11,000 hadi zaidi ya tani 40,000 na mapato ya wakulima kufikia zaidi ya shilingi bilioni 40.480.